dev.kisakuzi.com, Moshi
HALI ya usafiri katika mkoa wa Kilimanjaro imeendelea kuwa mbaya baada ya madereva kukaidi agizo la serikali lililowataka kuendelea na kazi wakati malalamiko yao kutaka kushushwa kwa ushuru yakiendelea kushughulikiwa na badala yake wameendelea na mgomo kwa siku ya nne mfululizo.
Hali hiyo imesababisha usumbufu mkubwa kwa wasafiri huku chama cha wasafirishaji mkoa wa Kilimanjaro na Arusha (AKIBOA) kikitupa lawama kwa viongozi wa wilaya na manispaa ya Moshi kushindwa kutatua kero yao hadi kuwafanya kuendelea na mgomo.
Akizungumza mwenyekiti wa AKIBOA, Husen Mrindoko alisema wameamua kuendelea na mgomo ikiwa ni kutii agizo la mkuu wa wilaya ya Moshi Dk. Ibrahim Msengi na kaimu mkurugenzi wa manispaa ya Moshi Dk. Christopher Mtamakaya lililowataka kama hawawezi kulipa ushuru uliopangwa wa Sh. 1,500 kwa magari madogo na Sh. 2,000 kwa magari makubwa kupaki magari yao nyumbani.
“Jana (Juzi) tulikaa ofisini kwa mkuu wa wilaya zaidi ya saa mbili kutafuta muafaka wa suala hili lakini hatukuweza kupata suluhu na badala yake mkuu wa wilaya alituambia kuwa kama hatuwezi kuendelea na kazi ya usafiri tukapaki magari yetu nyumbani na sasa tumetii hilo ila tunawaomba abiria watusamehe sana kwa usumbufu huu hatujapenda sisi utokee,” alisema Mrindoko.
Aizungumzia suala hilo kaimu mkurugenzi wa manispaa ya Moshi Dk. Christopher Mtamakaya alisisitiza kuwa mapitio ya marekebisho ya sheria ya ushuru wa magari ambayo imedumu kwa zaidi ya miaka tisa toka mwaka 2002 ilipitia mchakato wote na lengo ni kuweza kuboresha miundombinu wala si kuwaumiza wasafirishaji.
“Sheria hii ilikuwa inawataka wasafirishaji wa magari kulipa Sh. 1000 lakini katika vikao vyetu vya mwaka jana tulipitia ushuru huu na tukaona iko kuna haja ya sheria hii kurekebishwa na lengo ni kuweza kuboresha miundombinnu lakini si kwamba hatukuwashirikisha wadau wote walishrikishwa ingawa wengine hawakukubaliana na suala hilo,” alisema.
Akizungumza kaimu mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Dk. Ibrahimu msengi alisisitiza kuwa nchi inaendeshwa kwa mujibu wa sheria na taratibu na hakuna mwenye mamlaka ya kutengua sheria hivyo ni lazima wasafirishaji wakaheshimu sheria.
Dk. Msengi alisema biashara ni jambo la hiari hivyo ni lazima mtu anayetaka kufanya biashara akafuata sheria na taratibu za biashara husika na k ama hawezi hakuna wa kumlazimisha.
“Hulazimishwi mtu kufanya biashara ya daladala au basi ni hiari yake na kama unaona ushuru uliopangwa unakukwaza achana na biashara hiyo nenda katafute bishara nyingine ambayo unaona inakufaa na si kufanya mgomo,” alisema Dk. Msengi.
Aidha Dk. Msengi alisema Serikali haitawafumbia macho wale wote ambao wanajiingiza kwenye vitendo vya vurugu kwa kuharibu magari ya watu ambao wanataka kufanya kazi kwa hiari yao wakati Serikali ikiendelea na majadiliano na wadau wa usafirishaji.
Aliwataka wamiliki wa magari mkoani Kilimanjaro kufuata sheria na kwamba wale ambao wanahitaji kufanya kazi wafanye bila woga kwani serikali iko makini na itawalinda ili kuhakikisha amani na utulivu vinakuwepo.
“Kwa sasa lazima sheria ichukue mkondo wake kwa wale wote ambao watabainika kuwabugudhi kwa kuwapiga mawe wale ambao wamekubali kufanya kazi kwa kulipa ushuru wa Sh.1,500 na Sh. 2,000 kwani hapa hatutakuwa tayari kuona amani ikivunjika kwa sababu ya watu wachache,” alisema.
Hata hivyo mkuu huyo aliwataka wananchi kuwa wavimilivu katika kipindi kigumu cha mgomo wa magari wakati seriklai ikiendelea kushughulikia tatizo hilo na kwamba waondokane na mitazamo kuwa mgomo huo unachichewa na itikadi za kisiasa.
Mgomo wa magari madogo na baadhi ya magari makubwa yanayofanya safari zake katika maeneo mbalimbali mkoani Kilimanjaro na Arusha ambao ulianza toka julai sita mwaka huu kutokana na kupandishwa kwa Ushuru kutoka Sh. 1,000 hadi 1,500 kwa magari madogo na sh. 2,000 kwa magari makubwa umesababisha adha kubwa kwa wasafiri huku jeshi la polisi likipata kazi ya kuzunguka maeneo mbalimbali kufanya doria na kuimarisha ulinzi.