MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imetabiri maafa makubwa yakiwamo mafuriko, mmomonyoko wa ardhi na uharibifu wa mazingira katika baadhi ya maeneo wakati wa wa mvua za vuli zinazotarajiwa kuanza mwezi huu hadi Desemba. Wakati TMA ikionya baadhi ya maeneo kukumbwa na athari hizo kutokana na kutarajiwa kupata mvua juu ya wastani, baadhi ya maeneo yanatarajiwa kukumbwa na uhaba wa chakula kutokana na kupata mvua chini ya wastani.
Kaimu Mkurugenzi wa TMA, Dk Agnes Kijazi aliwaambia waandishi wa habari Dar es Salaam jana kuwa mamlaka zinazohusika na huduma za afya hazina budi kuchukua tahadhari na kuweka maandalizi stahiki ya kupambana na magonjwa ya milipuko kutokana na mabadiliko hayo ya hali ya hewa.
Dk Kijazi alisema maeneo ya mashariki mwa Ziwa Victoria, Pwani ya Kaskazini, Visiwa vya Unguja na Pemba na Magharibi mwa Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki, yatakuwa na mvua za wastani na juu ya wastani katika maeneo mengi.
Alisema mvua za vuli katika maeneo ya kaskazini mwa nchi, zinatarajiwa kuanza katika wiki ya pili ya mwezi huu katika Kanda ya Ziwa Victoria na kuendelea kusambaa katika maeneo mengine yanayopata mvua misimu miwili kwa mwaka. Dk Kijazi alisema, Mikoa ya Kagera, Mara, Mwanza, Shinyanga na kaskazini mwa Mkoa wa Kigoma, mvua zilitarajiwa kuanza katika wiki ya pili ya mwezi huu, zikiwa juu ya wastani.
Kuhusu Mikoa ya Pwani, Dar es Salaam, Tanga, Morogoro (Kaskazini – Mashariki) na katika Visiwa vya Unguja na Pemba, alisema mvua zinatarajiwa kunyesha katika kiwango cha juu ya wastani. Dk Kijazi alisema katika Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki, ambayo ni Mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara, mvua zinatarajiwa kuanza katika wiki ya tatu ya Oktoba akisema zitakuwa juu ya wastani.
Alisema Kanda za Magharibi, Kati, Juu Kusini Magharibi na Mikoa ya Kusini na Pwani ya Kusini, mvua zinatarajiwa kuwa za wastani na juu ya wastani katika maeneo mengi.
“Maeneo ya Lindi na Mtwara na mashariki mwa Mkoa wa Ruvuma, yanatarajiwa kuwa na mvua za wastani katika kipindi chote cha Vuli,” alisema. Alisema Mikoa ya Tabora, Rukwa na Kigoma itakuwa na mvua kuanzia wiki ya tatu na ya nne ya Novemba na zinatarajiwa kuwa za wastani na juu ya wastani. Dk Kijazi alisema Mikoa ya Singida na Dodoma inatarajiwa kupata mvua katika wiki ya tatu ya Novemba ambazo zitakuwa juu ya wastani.
Dk Kijazi pia alisema Mikoa ya Mbeya, Iringa na Morogoro – Kusini inatarajia kupata mvua wiki ya tatu ya Novemba ambazo zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani. Mikoa ya Ruvuma, Mtwara na Lindi alisema inatarajiwa kupata mvua kuanzia wiki ya nne ya Novemba na zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani. Alisema mvua hizo pia zitakuwa za juu ya wastani katika maeneo ya magharibi mwa Ruvuma.
Maeneo yenye hatari ya njaa Dk Kijazi alisema maeneo yatakayopata mvua chini ya wastani, ndiyo yatakayokabiliwa na uhaba wa chakula na njaa. Alitaja maeneo hayo kuwa ni pamoja na Mkoa wa Mtwara, maeneo ya mashariki wa Ruvuma na Kusini mwa Mkoa wa Lindi.
Kaimu Mkurugenzi huyo wa TMA alisema katika maeneo mengi ya nchi yanayotarajiwa kuwa mvua za kutosha, wakulima wanashauriwa waendelee na taratibu kawaida za kilimo.
“Maeneo yanayotarajiwa kupata mvua juu ya wastani unyevunyevu wa udongo kupita kiasi unaweza kuathiri maendeleo ya mazao, Mamlaka inawashauri wakulima waendelee kutafuta ushauri wa maofisa ugani,” alisema.
Alisema hali ya malisho ya mifugo inatarajiwa kuimarika katika maeneo mengi nchini, hivyo wafugaji wazingatie ushauri kutoka kwa maofisa wa mifugo katika maeneo yao. Kuhusu maji na nishati, alisema upatikanaji wa maji nchini unatarajiwa kuwa wa kutosheleza katika maeneo mengi, hivyo kusisitiza usimamizi pamoja na mbinu za kuvuna maji kadri inavyowezekana.
“Hizi mvua zitasaidia mabwawa mengi kutajaa, ila izingatiwe kuwa vina vya maji viko chini hivyo ongezeko hilo halitarajiwi kumaliza upungufu uliopo,” alisema. Dk Kijazi alizishauri mamlaka zinazohusika na masuala ya afya kuchukua tahadhari na kuweka maandalizi stahiki ya kupambana na mlipuko wa magonjwa utakaotokana na mabadiliko hayo ya hali ya hewa.
CHANZO: Mwananchi