Hakuna tena Tsunami Tanzania – TMA

Bendera ya Tanzania

Na Mwandishi Wetu, dev.kisakuzi.com

MAMLAKA ya Utabiri wa Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imesema hakuna tena tishio la kutokea kwa tsunami iliyotarajiwa kutokea maeneo ya pwani mwa Bahari ya Hindi.

Awali TMA kwa kushirikiana na mamlaka za utabiri kutoka nje ya nchi zilitabiri kutokea kwa tsunami katika maeneo hayo jambo ambalo lilizua hofu na woga kwa wakazi wengi wa Tanzania hasa pwani mwa Bahari ya Hindi.

Kwa mujibu wa taarifa ambayo TMA imeitoa asubuhi hii ni kwamba hakuna tena dalili za kutokea kwa tsunami hiyo kama iliyokuwa imetabiriwa awali.

“Tunaomba wananchi waendelee na shughuli zao kama kawaida kwani inaonekana hakuna tena tishio la kuzuka kwa tsunami kama tulivyokuwa tumetabiri awali,” kimesema chanzo kimoja cha habari kutoka mamlaka ya hali ya hewa Tanzania asubuhi hii.

Kuanzia jana shughuli za kusafirisha abiria kutoka Dar es Salaam kwenda mjini Zanzibar zilisitishwa kwa kuhofia kuzuka kwa tsunami katika Bahari ya Hindi, jambo ambalo lilisimamisha baadhi ya shughuli maeneo kadhaa ya Jiji la Dar es Salaam.