
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Willium Lukuvi, akimkabidhi hati ya umiliki wa ardhi na makazi mmoja wa wakazi wa Kata ya Buhongwa Jijini Mwanza ambaye makazi yake yamerasimishwa kutoka makazi holela baada ya zoezi la upimaji kufanyika.
Na George Binagi, Mwanza
WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Willium Lukuvi, ameziagiza halmashauri za Jiji la Mwanza na Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza, kuhakikisha zinakamilisha zoezi la upimaji na urasimishaji makazi yaliyojengwa kiholela hadi ifikapo june 30 mwakani.
Waziri Lukuvi ametoa agizo hilo hii leo Jijini Mwanza alikofanya ziara ya kujionea utekelezaji wa urasimishaji makazi yaliyoendelezwa kiholela Jijini Mwanza ambapo amebainisha kwamba Serikali haina mpango wa kuwavunjia wananchi makazi yaliyojengwa kiholela na badala yake imeandaa mpango huo ili kutambua makazi hayo na kuwapatia wananchi hati miliki ya makazi yao.
Aidha amewatahadharisha wananchi kwamba, mpango wa kurasimisha makazi yaliyojengwa kiholela hautayahusisha makazi yaliyojengwa kwenye maeneo hatarishi ikiwemo kwenye mabonde, miinuko, mafuriko pamoja na hifadhi za barabara.
Baadhi ya wananchi Jijini Mwanza ambao makazi yao yamerasimishwa na kupewa hati ya umiliki, wameipongeza serikali kwa hatua hiyo ambapo wameomba kasi ya zoezi hilo kuongezeka ili wananchi zaidi ya elfu 35 ambao makazi yao hayajapimwa, yaweze kupimwa na kupatia hati za umiliki kwa wakati kama Waziri Lukuvi alivyoagiza.
Mkuu wa mkoa wa Mwanza, John Mongella, amemuhakikishia Waziri Lukuvi kwamba hadi kufikia mwezi Januari mwaka ujao, zoezi la kupima makazi yaliyojengwa kiholela na kuyarasimisha katika Jiji la Mwanza na Maspaa ya Ilemela, litakuwa limekamilika.