Hakuna atayeporwa ardhi Tanzania – Rais Kikwete

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete


Na Mwandishi Wetu

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa hakuna hata inchi moja ya ardhi ya mkulima mdogo katika Tanzania itaporwa ili wapewe wawekezaji wa kigeni chini ya mpango kabambe wa kuleta mageuzi makubwa katika kilimo cha Tanzania.

Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa ni unafiki kwa baadhi ya wanasiasa kusema kuwa wanaamini katika umuhimu wa kukaribisha wawekezaji nchini lakini wakati huo huo wanahubiri siasa za uchochezi dhidi ya wawekezaji hao.

Rais Kikwete ameyasema hayo Juni 7, 2012, wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Canada katika Tanzania, Robert J. Orr, ambaye anamaliza muda na uwakilishi wake nchini na amemwaga Rais Kikwete akijiandaa kurejea kwako.

Baada ya kuulizwa na Balozi Orr kuhusu jinsi gani anaona mchango wa sekta binafsi katika kuendeleza na kukuza uchumi wa Tanzania, Rais Kikwete amesema kuwa angependa kuona uwekezaji mkubwa zaidi nchini kwa sababu ni uwekezaji mkubwa zaidi ndio utakuza uchumi kwa kasi zaidi na hivyo kuchangia kuleta maisha bora zaidi kwa wananchi.

Hata hivyo, Rais Kikwete amesema kuwa zipo changamoto katika kukaribisha wageni ikiwa ni pamoja na mawazo ya baadhi ya watendaji na hata viongozi ambayo hajabadilika sana kutokana na miaka mingi ya utekelezaji wa siasa ya Ujamaa na uchochezi wa baadhi ya wanasiasa dhidi ya wawekezaji.

“Wapo watu, kwa mfano, wanachochea wananchi wakisambaza uongo kuwa Serikali inakusudia kupora ardhi ya wakulima wadogo ili kuwapa wawekezaji wakubwa katika dhamira yetu ya kuleta mageuzi makubwa ya kilimo nchini. Huu ni upotoshaji wa makusudi kwa sababu hakuna hata inchi moja ya ardhi ya mkulima mdogo itachukuliwa na Serikali. Wawekezaji wakubwa watapatiwa ardhi kutoka kwenye Benki ya Ardhi ambako kila wilaya inatenga ardhi kwa ajili ya madhumuni hayo,” amefafanua Rais Kikwete.

Ameongeza; “Wapo pia wanasiasa wanahubiri sera zisizotekelezeka. Upande mmoja wanalaumu kuwepo kwa umasikini nchini, lakini Serikali inapokaribisha wawekezaji ili kuboresha uchumi na kumaliza umasikini huo wanageuka na kuchochea wananchi kuwa wawekezaji hawafai wanakuja kupora ardhi ya wananchi.”

Amesisitiza: “Uzuri ni kwamba kuhusu hili, Serikali ina sera iliyo wazi na dhamira thabiti ya kuendelea kukaribisha wawekezaji kuingia katika uchumi wa Tanzania na kuchangia maendeleo ya nchi yetu kwa sababu hakuna uchumi wowote duniani unaokua bila kupata wawekezaji wa ndani na nje.”

Alipoulizwa na Balozi kuhusu matukio ya baadhi ya wananchi kuvamia migodi ya baadhi ya makampuni makubwa, Rais Kikwete amesema: “Huwezi kuchochea makundi ya watu kuvamia migodi na ukatarajia kuwa hapatawepo na hatua dhidi ya makundi hayo.”