Hakimu Arusha atishia ‘kuifuta’ kesi ya Lema

Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (CHADEMA)

Na Mwandishi Wetu, Arusha

HAKIMU Judith Kamala anayesikiliza kesi inayomkabili Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (CHADEMA) na wafuasi 18 wa Chama hicho, amemuonya Mwendesha Mashitaka wa Serikali, Augustino Kombe kuhakikisha anazingatia muda wa kesi vinginevyo Mahakama
itaifuta kesi hiyo.

Hakimu Kamala aliyasema hayo jana mahakamani mjini hapa kabla ya kuamua kuahirisha shauri hilo hadi Februari 29, 2012 saa nne asubuhi, itakapoanza kusikilizwa maelezo ya awali.

Onyo hilo lilifuatia malalamiko ya mmoja wa watuhumiwa katika kesi
hiyo aliyeiomba mahakama kuzingatia muda kwa sababu wamekuwa wakifika mapema mahakamani hapo na kukaa kwa muda mrefu bila kesi hiyo kuanza.

Alitolea mfano leo kesi hiyo ilitakiwa kuanza kusikilizwa asubuhi lakini ilisikilizwa kuanzia saa 6 mchana bila sababu za msingi.

Hakimu Kamala amesema kesi hiyo ilichelewa kutokana na Mwendesha Mashitaka wa Serikali kuchelewa kufika mahakamani, hivyo akamtaka itakapotajwa tena kuwahi na endapo atachelewa muda uliopangwa ataifuta kesi.

Hata hivyo kesi hiyo ambayo ilikuwa imepangwa kuanza kusikilizwa leo baada ya upelelezi kukamilika, imekwama baada ya Lema kushindwa kufika mahakamani. Kwa mujibu wa mdhamini wake aliieleza mahakama kuwa Lema ni mgonjwa anasumbuliwa na tumbo hivyo amekwenda hospitali kwa ajili ya matibabu.

Mwendesha Mashitaka wa Serikali, Rose Sulley leo ameiomba mahakama hiyo kupanga tarehe ya kuanza kusikiliza maelezo ya awali ya kesi hiyo baada ya upepelezi wake kukamilika. Katika shauri hilo washitakiwa wote wanakabiliwa na makosa anuai huku Lema akikabiliwa na makosa matano.

Kosa la kwanza linawakabili watuhumiwa hao ni njama ya kutenda kosa
kinyume cha sheria ya kifungu nambari 384 na 385 cha kanuni ya
adhabu, kosa la pili ni kufanya maandamano yasiyo halali ambayo yalianzia katika barabara ya mahakama ya hakimu mkazi mkoani hapa hadi kwa mkuu wa wilaya ya Arusha, zilipo ofisi za Mbunge huyo.