Hakimu Aachiwa Huru Mashitaka ya Rushwa

Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Ilala, Pamela Kalala

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuachia huru Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Ilala, Pamela Kalala baada ya kumuona hana kesi ya kujibu katika kesi ya rushwa iliyokuwa ikimkabili. Kalala aliachiwa huru jana na Hakimu Mkazi Aloyce Katemana baada ya kupitia ushahidi wa mashahidi saba wa upande wa mashtaka uliotolewa mahakamani hapo.

“Upande wa mashtaka ulikuwa na mashahidi saba, inadaiwa mshtakiwa aliomba na kupokea rushwa ili iwe kishawishi cha kumsaidia mshtakiwa katika kesi ya jinai.

“Inadaiwa baada ya kuwasilishwa malalamiko kwa mahakama ya juu ilibainika kwamba alifuta dhamana ya mshtakiwa bila kutoa sababu.

“Ushahidi unaonyesha kwambe mke wa mshtakiwa aliyefutiwa dhamana, Josephine Wage hakulalamika kwamba aliombwa rushwa bali alilalamikia mwenendo wa kesi na kufutiwa dhamana kwa mumewe,”alisema Katemana.

Alisema kutokana na ushahidi huo inawezekana Hakimu Kalala kwa uzembe alishindwa kueleza sababu za kumfutia dhamana mshtakiwa.

“Kutokana mashtaka yanayomkabili na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka, mahakama inamuona mshtakiwa hana kesi ya kujibu na mashtaka yote matatu ya rushwa dhidi yake yanatupiliwa mbali,”alisema Hakimu Katemana.

Hakimu Kalala alifunguliwa kesi namba 223 ya 2012, anadaiwa kuomba rushwa ya Sh milioni tatu na kupokea Sh 900,000.

Inadaiwa kwamba katika tarehe tofauti Februari mwaka jana jijini Dar es Salaam, mshtakiwa aliomba rushwa ya Sh milioni tatu kutoka kwa Josephine Wage, ambaye ni mke wa mmoja wa washtakiwa wa kesi ya jinai.

Kesi hiyo ni ya Jamhuri dhidi ya Abubakari Mzirahi na wenzake na ilidaiwa Hakimu Kalala aliomba fedha hizo iwe kishawishi cha kutoa upendeleo kwa mume wa Wage wakati wa kutoa hukumu.

CHANZO: www.mtanzania.co.tz