Na Joachim Mushi, dev.kisakuzi.com
TAASISI ya HakiElimu nchini imeishauri Serikali pamoja na Chama Cha Walimu Tanzania (CWT) kufikia makubaliano haraka iwezekanavyo, ili kumaliza mgomo uliopo kwani waathirika zaidi na mgomo huo si wao bali ni ni wanafunzi.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa HakiElimu, Bi. Elizabeth Missokia alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kuhusiana na mgomo wa walimu unaoendelea maeneo mbalimbali nchini.
Alisema kila mwanafunzi ana haki ya kujifunza na kuelimishwa, kitu ambacho hawakipati kwa sasa kutokana na mgomo wa walimu wanaoshinikiza Serikali iwaongeze mishahara pamoja na kuwaboreshea mazingira ya kazi zao.
Mkurugenzi huyo alisema kauli ya Serikali kudai haina uwezo wa kuboresha maslahi na mazingira ya kazi ya watumishi wake haileti unafuu wa maisha kwa watumishi wa umma hivyo kushauri iangalie namna ya kufanya kumaliza mgogoro huo.
“HakiElimu inasisitiza kwamba nchi itafanikiwa kuboresha elimu endapo tu itawekeza kwa walimu kwa kuboresha mazingira ya kazi, maslahi ya walimu, kuwashirikisha walimu katika maamuzi kuhusu masuala ya elimu na kuwapa walimu mafunzo kazini. Elimu bora haiwezi kuletwa na walimu walio hoi,” alisema Missokia.
Aidha amewataka walimu kuhakikisha wanadai haki zao huku wakiendelea kuwajibika kwa kufundisha na kuendeleza elimu yetu, kwani wanamgogoro na Serikali na wala si wanafunzi na jamii kwa ujumla.
“HakiElimu inawakumbusha walimu kuwajibika. Wadai haki zao, huku wakitimiza wajibu wao wa kufundisha na kuendeleza elimu yetu. Wafundishe kwa bidii bila kinyongo, kwa kuwa wasipowajibika watakuwa wanawaumiza wanafunzi na jamii kwa ujumla. Mgogoro uliopo ni baina yao na Serikali, na si wanafunzi,” alisema Mkurugenzi huyo Mtendaji.
“Viongozi wa Serikali wasiwabeze walimu; kwa kufanya hivyo wanawakatisha tamaa. Hata kama baadhi ya walimu hawakusoma kwa miaka mingi kama ilivyo kwa fani nyingine, wana umuhimu mkubwa sana. Ndio wanaowaandaa watanzania wa leo na kesho kimtazamo na kimaarifa. Hivyo, kudai kuboreshewa mazingira ya kazi ni haki yao; na Serikali inaweza kutimiza wajibu wake kwa kuwasikiliza na kushauriana nao bila ubabe na kejeli,” alisema.
Pamoja na hayo ameliomba Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuingilia kati mgogoro huo na kutenga muda kujadili suala hilo kwa kina ikiwa ni pamoja na kuishauri serikali, hasa kuhusu tahadhari za kuchukua ili tatizo kama hili lisitokee tena.
“Bunge lina wajibu wa kuishauri na kuisimamia Serikali kuhusu sera, utendaji na usimamizi wa elimu nchini. Inasikitisha kwamba Bunge linakwepa kujadili tatizo hili kwa maelezo kwamba liko mahakamani. Tunaamini kwamba mahakama italiangalia suala hili na kutenda haki, lakini wajibu wa Bunge uko pale pale…” alisema Bi. Missokia.
Amekiri kwamba ni kweli gharama za maisha zinazidi kupanda, huku mfumuko wa bei nao unaendelea kuwaumiza watumishi kila siku, hivyo kuishauri Serikali kutafuta vyanzo mbadala vya mapato ili kuweza kuwaboreshea mapato watumishi wake.
“Serikali ijijengee utaratibu wa kuboresha mazingira ya watumishi wake, na si kusubiri kwenda mahakamani kuzuia watumishi kugoma. Watumishi wa umma watafanya kazi kwa ari endapo tu wameridhika na mazingira ya kazi na maslahi yao; na si kwa kutumia uamuzi wa mahakama peke yake.”
Habari hii imeandaliwa na Mtandao wa dev.kisakuzi.com (www.thehabari.com)