Hadhi ya Tanzania Yapanda Katika Benki ya Afrika

Mwakilishi Mkazi wa Benki hiyo katika Tanzania, Bi. Tonia Kandiero

Mwakilishi Mkazi wa Benki hiyo katika Tanzania, Bi. Tonia Kandiero

TANZANIA imepandishwa hadhi katika Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na sasa inaweza kupata mikopo mikubwa zaidi na yenye hadhi kubwa zaidi kuliko huko nyuma. Mwakilishi Mkazi wa Benki hiyo katika Tanzania, Bi. Tonia Kandiero ametangaza hayo, Julai 23, 2014.

Bi. Kandiero amesema kuwa miaka yote tokea Tanzania kuwa mwanachama wa AfDB, imekuwa inapata mikopo ya hadhi ya chini zaidi na midogo zaidi ya maendeleo kutokana na uwezo na nguvu za uchumi wake. Amesema kuwa hadhi ya Tanzania ndani ya Benki hiyo imepanda kutokana na kukua kwa uchumi wa Tanzania, kuongezeka kwa uwezo wa kukopesheka na uwezo wa kulipa na kutimiza masharti yanayokwenda na mabadiliko hayo ya hadhi.

Bi. Kandiero ametangaza mabadiliko hayo katika hadhi ya Tanzania ndani ya Benki hiyo wakati alipozungumza katika sherehe kubwa ya kuweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa Barabara ya Mangaka-Mtambaswala kwa kiwango cha lami na kufungua Barabara ya Masasi-Mangaka ambayo imekamilika kwa kiwango cha lami.

Barabara zote ziko katika mkoa wa Mtwara na mgeni rasmi katika sherehe hiyo kubwa iliyofanyika mjini Mangaka, mji mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu, alikuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa
Jakaya Mrisho Kikwete, ambaye ameingia Mkoani Mtwara jana kwa ziara ya siku mbili. Ameingia Mtwara akitokea Ruvuma ambako alifanya ziara ya siku sita.

Bi. Kandiero amemwambia Rais Kikwete na mamia ya wananchi waliohudhuria sherehe hiyo kuwa kabla ya kupandishwa hadhi, Tanzania ilikuwa na sifa za kukopa ndani ya benki hiyo mikopo kutoka Mfuko wa Maendeleo wa Benki hiyo na siyo mikopo mikubwa ya maendeleo.

Bi. Kandiero amesema kuwa tokea Tanzania kujiunga na AfDB imepata kiasi cha mikopo ya thamani ya zaidi ya dola za Marekani bilioni moja. AfDB ni moja ya wafadhili wa barabara hizo mbili ambazo sherehe zake za uzinduzi na jiwe la msingi zimefanyika jana kwa kushirikiana na Serikali ya Japan kupitia Shirika la Maendeleo la Japan (JICA) na Serikali ya Tanzania.

AfDB na JICA zinashirikiana na Serikali ya Tanzania kugharimia ujenzi wa barabara hizo chini ya Mradi wa kuendeleza Barabara nchini. Chini ya ushirikiano huo, AfDB inatoa asilimia 64.79 kugarimia ujenzi wa barabara hizo, JICA inatoa asilimia 31.83 na Serikali ya Tanzania inatoa asilimia 2.39.
Barabaraba ya Mangaka-Mtambaswala, mpakani mwa Tanzania na Mozambique, ina urefu wa kilomita 65.5, inajengwa na kampuni ya Jamhuri ya Watu wa China kwa gharama ya shilingi bilioni 59.66 na ujenzi utakuchukua miezi 28.

Nayo Barabara ya Mangaka-Masasi yenye urefu wa kilomita 55.1 ilikamilika mwanzoni mwa mwaka huu baada ya kuwekewa jiwe la msingi la ujenzi wake na Rais Kikwete Agosti 21, 2009. Barabara hiyo, ilijengwa na kampuni kutoka Japan kwa awamu tatu na kwa gharama ya shilingi bilioni 54.8. Barabara hiyo ni sehemu ya barabara ya Masasi-Mangaka-Tunduru. Mapema jana, Rais Kikwete amezindua mradi wa maji wa Tarafa ya Nalasi mkoani Ruvuma mjini Nalasi, kilomita 12 kutoka mpakani mwa Tanzania na Mozambique.

Mradi huo ambao ni moja ya miradi inayofadhiliwa na Benki ya Dunia utawanufaisha watu 11,655 katika vijiji vitatu. Mradi huo una uwezo wa kutoa lita 200,000 za maji ambayo yataweza kupatikana katika vituo 37 vya ugawaji maji. Ili kusambaza maji hayo kwa watu wengi zaidi, kiasi cha kilomita 14.5 ya mabomba yametandazwa katika vijiji hivyo. Mradi huo umejengwa na Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru kwa gharama ya sh milioni 445.