COSTECH YATOA MAFUNZO YA KILIMO CHENYE TIJA KWA WAKULIMA KATIKA MAONYESHO YA NANENANE MKOANI LINDI

Mwezeshaji kutoka Jukwaa la Bioteknolojia Tanzania (OFAB), Dk. Emmarold Mneney (kulia), akitoa mafunzo ya siku moja ya kilimo chenye tija  kwa wakulima wa Mkoa wa Lindi kwenye Maonyesho ya Kitaifa ya Nanenane yanayoendelea kwenye viwanja vya Ngongo mkoani hapa leo.

Wakulima wakiwa kwenye mafunzo hayo.
Usikivu katika mafunzo hayo yaliyofanyika Ukumbi wa Mikutano katika Jengo la Halmshauri ya Wilaya ya Kilwa lililopo katika viwanja hivyo vya Ngongo.
Mafunzo yakiendelea.
Mkulima kutoka Wilaya ya Kilwa, Omari Kijuwile akichangia jambo kwenye mafunzo hayo.
Dadi Uredi Chibwana mkulima kutoka Kijiji cha Kiwalala Lindi Vijijini akielezea changamoto mbalimbali walizonazo wakulima katika mkoa huo.
Mkulima Zarafi Mahamudu kutoka Manispaa ya Lindi, akizungumza kwenye mafunzo hayo.
Anastazia Benjamin Lai kutoka Wilaya ya Kilwa akitoa shukurani kwa COSTECH kwa kuwapelekea mafunzo hayo.
Mratibu wa Jukwaa la Bioteknolojia kwa Maendeleo ya Kilimo (OFAB), Dk.Philbert Nyinondi ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kilimo Morogoro (SUA), akiwaelezea wakulima hao umuhimu wa matumizi ya MB katika siku zao katika kuinua kilimo na utafutaji wa masoko katika maeneo mengine ya ndani na nje ya nchi.
 
Na Dotto Mwaibale, Lindi
 
TUME ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) imetoa mafunzo ya siku moja kwa wakulima wa Mkoa wa Lindi yenye lengo la kuwasaidia kulima kilimo chenye tija.
 
Mafunzo hayo yametolewa na mwezeshaji kutoka Jukwaa la Bioteknolojia kwa maendeleo ya Kilimo (OFAB), Dk. Hamalord Mneney katika maonyesho ya kitaifa ya wakulima Nanenane yanayoendelea Viwanja vya Ngongo mkoani hapa leo.
 
Akizungumza kuhusu mafunzo hayo Dk. Mneney alisema Serikali imeona itoe mafunzo kwa wakulima hao ili wajifunze kilimo cha kisayansi chenye tija badala ya kuendelea na kilimo cha mazoea.
 
“Serikali siku zote inawajali wakulima ndio maana tukaona ni vizuri kuleta mafunzo haya kwa hawa wakulima ili kuondoa changamoto wanazokabiliana nazo katika shughuli zao za kilimo” alisema Dk.Mneney.
 
Wakulima walionufaika na mafunzo hayo ni kutoka wilaya za Lindi, Lindi vijijini, Rwanga, Kilwa na Nachingwea ambapo kulikuwa na washiriki zaidi ya 20.
 
Wakizungumza katika mafunzo hayo wakulima hao walisema changamoto kubwa waliyonayo  ni mabadiliko ya tabia nchi na ukame unaotokana na mvua kutopatikana kwa wakati pamoja na pembejeo za kilimo kutowafikia kwa wakati.
 
Walitaja changamoto nyingine kuwa ni mazao ya chakula kushambuliwa na wadudu waharibifu, kukosekana kwa masoko ya mazao yao na magonjwa kama batobato na michirizi kahawia yanayoshambulia mihogo pamoja na mbegu bora.
 
Mkulima Omari Kijuwile kutoka Wilaya ya Kilwa alisema wakulima wana ari ya kulima lakini wanakosa mtaji baada ya taasisi za kifedha kushindwa kuwakopesha kwa kuwa hawana kitu cha kuweka dhamana ambapo aliomba umilikishwaji wa mashamba yao kwa hati za kimila ambazo zitatambuliwa na taasisi hizo ili waweze kupata mikopo hiyo.
 
“Tunaomba tumilikishwe mashamba yetu kwa hati za kimila ili tuweze kuaminika na kupata mikopo kutoka taasisi za kifedha” alisema Kijuwile.
 
Mkulima Dadi Uredi Chibwana kutoka Kijiji cha Kiwalala Lindi vijijini ni vizuri wakulima wakajenga tabia ya kufuata ushauri wa maofisa ugani kuhusu kilimo badala ya kutegemea kilimo cha mazoea.
 
Zarafi Mahamudu mkulima wa Manispaa ya Lindi alisema wakulima wamekuwa wakijitahidi lakini masoko yamekuwa ni changamoto kubwa kwao hivyo aliiomba serikali kuangalia jambo hilo kwa undani zaidi.
 
Mkulima kutoka Wilaya ya Kilwa Anastazia Lai aliomba serikali na wadau wengine itoe msaada wa kukabiliana na wadudu waharibifu wa mazo badala ya kuacha nguvu zao kupotea bure kutokana na wadudu hao.
 
Mratibu wa Jukwaa la Bioteknolojia kwa Maendeleo ya Kilimo (OFAB), Dk.Philbert Nyinondi ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kilimo Morogoro (SUA), aliwataka wakulima hao kutumia simu zao kutafuta masoko badala ya kutumia kwa matumizi yasiyo na tija.
 
“Wenzenu wa nchi zingine wamekuwa wakitumia MB katika simu zao kuwasiliana na wakulima wa nchi zingine katika masuala ya kilimo na kutafuta masoko ya mazo yao badilikeni nanyi mnaweza kufanya hivyo” alisema Dk. Nyinondi.