Hab Mkwizu Awapa Somo Wajumbe Bodi ya Mishahara

Minister of State in the President’s Office for Public Service and Management, Hawa Ghasia

Na Magreth Kinabo – MAELEZO

KAIMU Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Hab Mkwizu amewataka Wajumbe Bodi ya Mishahara na Masilahi katika Utumishi wa Umma, kuwa na uhusiano na ushirikiano endelevu utakaolenga kutoa ushauri mzuri kwa bodi na serikali ili kuboresha mishahara na utendaji katika utumishi huo.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Katibu Mkuu huyo wakati akifungua mkutano wa siku mbili wa bodi hiyo unaohusisha wakuu wa idara, vitengo vya utawala na usimamizi wa rasilimali watu kutoka utumishi huo unaofanyika hoteli ya Blue Pearl jijini Dares Salaam.

“Wakati wa kujadili suala hili, itabidi kuangalia kwa kina ili muone jinsi ya kutumia nafasi zenu kutumia mifumo iliyopo ili kuhakikisha kuwa masihali na tija havitenganishwi aua lugha nyingine haki na wajibu vinaunganishwa ipasavyo,” alisema Mkwizu.

Katibu Mkuu huyo alisisitiza kuwa kama masilahi hayataendana na tija yatakuwa si endeleavu na yanaweza kuwa chnazo cha migogoro kati ya serikali na wanayakazi, hilo likitokea huduma zitasimama na nchi itakuwa kwenye tatizo la kutotoa huduma. Alisema mkutano huo utakuwa na tija iwapo wajumbe watatoa michango na mapendekezo yao ambayo yatasaidia bodi kuishauri serikali.

Aidha alisema kwa kipindi kirefu kumekuwa na malalamiko mengi katika utumishi na misingi yake pamoja na sababu nyingine ni tofauti ya kipato au kile kinachooneka kama ni mgawanyo usio wa haki wa rasilimali za taifa. Mkwizu aliongeza kuwa michango hiyo iwe endeleavu na bodi ianzishe utaratibu/mfumo wakupokea michango toka wa wadau na hasa kwa wao wenyewe.

Jumla ya mada sita zitajadiliwa katika mkutano huo, ambazo ni muundo na majukumu ya bodi, uhusinao na masilahi ya bodi, nafasi ya wakuu wa idara za utawala na usimamizi wa rasilimali watu katika kuboresha masilahi, hali ya uchumi na mwenendo wa mishahara, gharama za maisha na hali ya mishahara nchini na kupitia rasimu ya dodoso la kukusanya taarifa za gharama za maisha na hali ya mishahara.