Guantanamo Kufungwa

Huku wafungwa katika gereza la Guantanamo wakiendelea kujitesa kwa kugoma kula, Rais Barack Obama ameahidi tena kulishinikiza bunge la Marekani kulifunga gereza hilo.

Katika mkutano na waandishi wa habari jana Jumanne, rais Obama alisema nchi yake haiweze kuendelea kuwaweka watu hao katika eneo lisilo katika himaya ya nchi yoyote milele. Obama alibainisha hoja zake za kulifunga gereza hilo, akisema kuwa uendeshwaji wake umekuwa na gharama kubwa huku likikosa ufanisi, na kwamba linaathiri sifa ya Marekani katika jamii ya kimataifa, na kupunguza ushirikiano na washirika wake katika vita dhidi ya ugaidi.

Rais wa Marekani Barack Obama Obama alisisitiza kuwa ni muhimu kuelewa kuwa Guantanamo siyo muhimu kuifanya Amerika kuendelea kuwa salama. “Wazo kwamba tutaendelea kuliweka kundi la watu ambao hawajashtakiwa kwa muda mrefu, ni kinyume na utamaduni wetu na laazima jambo hilo likome,” alisema.

Ahadi isiyotekelezeka

Alipochaguliwa kuwa rais zaidi ya miaka minne iliyopita, Obama aliahidi kulifunga gereza hilo katika kipindi cha mwaka mmoja, lakini hakuchukulia kwa uzito, upinzani ambao ungetoka bungeni dhidi ya kuhamishwa kwa watuhumiwa wa ugaidi katika ardhi ya Marekani, na gharama za kuwapeleka wafungwa katika maeneo mengine, na hivyo hakuwa na njia isipokuwa kuliacha liendelee kutumika.

Kwa mujibu wa wizara ya sheria ya Marekani wafungwa 48 kati ya waliopo katika gereza la Guantamano hawawezi kushtakiwa kwa sababu waliteswa sana, na hawawezi kuachiwa kwa sababu wanachukuliwa kuwa ni hatari sana.

Obama pia alizungumzia juu ya suala la kuwalisha kwa nguvu, wafungwa waliogoma kula, jambo ambalo limelaaniwa na madaktari kuwa ni kinyume na maadili. “Sitaki watu hao wafe, ndiyo maana wizara ya ulinzi inajaribu kushughulikia hali hiyo kwa kadiri wanavyoweza. Lakini nadhani sote tunapaswa kujiuliza kwa nini tunafanya hivi.”

Wanaharakati wakiandamana mbele ya Ikulu ya WHite House wakimtaka Rais Obama afunge gereza la Guantanamo. Swali linaloulizwa na makundi ya haki za binaadamu ni kwa nini Obama alisaini sheria zilizopitishwa na bunge, ambazo zilifanya kufungwa kwa gereza la Guantanamo kuwa kinyume na sheria, au kuwahamisha wafungwa nchini Marekani.

“Nadhani rais alifanya kosa kwa kukubaliana na sera zinazohusu gereza la Guantanamo – tume za kijeshi, vifungo visivyo na kikomo, na kwa ujumla kuendelea kulifungua gereza la Guantanamo kama suala la kisera,” anasema Raha Wala kutoka shirika la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch.

Lakini hii ndiyo ahadi ya sera ambayo rais hakuweza kuitimiza katika mwaka wake wa kwanza wakati chama chake kilikuwa kinadhibiti mabaraza yote ya bunge. Na sasa anajaribu tena katika muhula wake wa pili, huku kukiwa na kiwango kidogo sana cha nia njema, na taifa ambalo hata rais mwenye anasema halionyeshi kujali.

-DW