WANAWAKE wapatao 15 hivi karibuni walihudhuria mafunzo ya kuongeza ujuzi wa jinsi ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi nchini Spain. Mafunzo na mradi huo vinafadhiliwa na Taasisi inayojihusisha na maendeleo ya wanawake wa Afrika, ijulikanayo kama Foundation for Women of Africa inayoongozwa na Makamu wa Rais mstaafu waSpain Mama María Teresa Fernández de laVega.
Taasisi hiyo itafanya kazi na wanawake hao 15 wa kitanzania kupitia miradi inayosaidia nchi kupambana na mabadiliko ya tabianchi. Wanawake hao ambao kati yao watano ni waandishi wa habari kila mmoja atatekeleza mradi mmoja, huku waandishi wa habari wakisaidia kupaza sauti za akinamama hao kupitia vyombo mbalimbali vya habari nchini.
Mradi huu unaojulikana kama GREEN VOICES una lengo la kupaza sauti za akinamama kueneza ujuzi wao wa kupambana na mabadiliko ya tabianchi ili jamii nzima ya kitanzania iweze kujifunza zaidi na kuzitumia mbinu hizo katika kupambana na mabadiliko ya tabianchi.
Mradi huo unaoratibiwa hapa nchini na Mtandao wa wanahabari wa Mazingira (EMNet) kwa niaba ya Foundation for Women of Africa unatekelezwa katika mikoa sita ya Kigoma, Kilimanjaro, Mwanza, Morogoro, Dar es Salaam na Pwani ukihusisha miradi ya kilimo, usindikaji, ufugaji na utafiti.
Mratibu wa EMNet Secelela Balisidya amesema akinamama hao wanatekeleza miradi ambayo inachangia moja kwa moja aidha kupambana au kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi. Amesema miradi hiyo ni mradi wa kilimo cha miti ya matunda mkoani Kigoma, kilimo cha viazi lishe visiwani Ukerewe mkoani Mwanza, Ufugaji Nyuki mkoani Morogoro na Pwani na ukaushaji wa mbogamboga kwa kutumia nishati ya jua mkoani Morogoro.
Miradi mingine ni usindikaji wa vyakula mbalimbali kutokana na muhogo mkoani Pwani, kilimo hai cha mbogamboga na kilimo cha uyoga mkoani Dar es Salaam, mradi wa majiko banifu mkoani Pwani na mradi wa utafiti wa jiko linalotumia nishati ya jua mkoani Kilimanajro.
Mradi huo unaotarajiwa kutelekezwa kwa mwaka mmoja unatoa fursa kwa kinamama kutoa ujuzo wao wa kupambana na mabadiliko ya tabianchi na sauti zao kusikika. Hiyo ni kwa sabuabu kinamama wana uhusiano mkubwa na mazingira kutokana na kazi wanazozifanya kila siku za kilimo na utunzaji wa familia kuhusiana moja kwa moja na mazingira hivyo kuyaelewa zaidi mazingira na jinsi ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi.
Wakiwa Madrid nchini Spain walikopata mafunzo wa wiki mbili katika chuo kikuu cha Autonomus Universitad De Madrid, akinamama hao na waandishi wa habari walijifunza kwa nadharia na vitendo jinsi nchi ya Spain inavyokabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuona njia ambazo na huku nchini zinaweza kutumika kupambana na mabadiliko ya tabianchi. Mafunzo kwa vitendo pia yalihusisha ziara za mafunzo kujifunza kilimo hai, na jinsi nishati jua inavyoweza kusaidia kupambana na mabadiliko ya tabianchi.
Waandishi wa habari pia walipata nafasi ya kutembelea chumba cha habari cha gazeti la Serikali ya Sapin la El Pais an kujifunza zaidi jinsi waandishi wa huko wanavyoandika habari zihusianazo na mabadiliko ya tabianchi.