WATU watano wote wakazi wa Kigogo Mbuyuni jijini Dar es Salaam wamefariki dunia baada ya kunywa pombe aina ya gongo, inayodhaniwa imechanganywa na spiriti ili kuifanya iwe kali zaidi.
Watu hao ambao watatu ni kutoka familia moja wamefariki dunia jana kwa nyakati tofauti ikiwa ni muda mfupi baada ya kunywa kinywaji hicho na sasa wengine watatu ambao nao walikunywa pombe hiyo wamelazwa katika Hospitali ya Amana wakiendelea na matibabu.
Taarifa ambazo mtandao wa dev.kisakuzi.com umezipata kutoka kwa mmoja wa majirani alisema watu hao walianza kulalamika maumivu ya tumbo baada ya kunywa gongo hiyo, huku wakiharisha na kutapika kabla ya kufariki dunia mmoja mmoja kadri walivyokuwa wakipelekwa kupata matibabu.
Waliofariki hadi sasa ni pamoja na vijana watatu wakiwemo Halid na Banzi (jina la kijana wa tatu halikupatikana mara moja), wazee wawili yaani mzee Juma na Upara.
Wengine ambao bado wamelazwa akiwemo anayedaiwa kuwa ni muuzaji wa pombe hiyo; Immakulata (Imma) ni pamoja na Mohamed na dada aliyetambuliwa kwa jina la Mama Steven. Baadhi ya majirani wamesema taarifa za awali katika nyumba hiyo zinadai pombe waliokunywa (gongo) ilikuwa imechanganywa na spiriti ili kuifanya iwe kali.
Taarifa zaidi kutoka eneo hilo zinasema nyumba ya familia ambayo ndiyo inadaiwa kuuza pombe hiyo ndiyo iliyoathirika zaidi kwani hadi sasa imepoteza wanafamilia watatu huku wawili akiwemo muuzaji wakiendelea na matibabu.
“Hadi sasa tuna maiti tatu ambazo hazijazikwa kutoka mtaa mmoja (Kigogo Mbuyuni karibu na Shule ya Msingi Rutihinda) hapa tunaomba Mungu wasiendelee kufa maana itakuwa kiama hapa mtaani kwetu,” alisema jirani mmoja ambaye hakupenda kutajwa mtandaoni.
Taarifa zaidi zimebainisha bado kuna baadhi ya watu ambao walikunywa pombe hiyo na wanaendelea kupata matibabu nyumbani huku wakihofia kwenda hospitalini kwani wanadai huenda wakakamatwa kwa unywaji wa pombe hiyo haramu.