Gianni Infantino Apewa Somo Yasimkute yale ya Blatter

5760

Rais mpya wa FIFA Gianni Infantino anakabiliwa na jukumu kubwa la kuleta mabadiliko na kuliunganisha soka la ulimwengu tangu aanze majukumu yake

Changamoto hizo ni rundiko la migogoro inayotokana na enzi ya Sepp Blatter iliyogubikwa na kashfa likihitaji kuchukuliwa hatua ya haraka.

Infantino, afisa mkuu katika shirikisho la kandanda la Ulaya – UEFA, ameahidi kuweka kikomo kwa siku za giza katika FIFA baada ya ushindi wake wa kishindo katika uchaguzi.

Lakini raia huyo Mswisi mwenye asili ya Kiitaliano tayari anakabiliwa na changamoto chungu nzima.

Wachezaji mahiri kabisa wa soka pamoja na washirika wakuu wa ufadhili lazima washawishike kuwa FIFA inaweza kuirekebesha nyumba yake.

Infantino pia atastahili kuyapa kipau mbele maslahi ya kuyaimarisha mataifa ya kandanda barani Asia na Afrika, mabara mawili ambayo yalimuunga mkono hadharani Sheikh Salman bin Ebrahim al-Khalifa wa Bahrain aliyemaliza katika nafasi ya pili kwa matumaini kuwa kiongozi asiyetoka Ulaya angeongoza FIFA baada ya urais wa miaka 18 ya rais wa Uswisi Blatter.