Gesi si Mwarobaini wa Umasikini, Kazi Shambani

Wakulima wa mpunga nchini India

Wakulima wa mpunga nchini India


Na Zitto Kabwe

TANZANIA kama ilivyo kwa Bara la Afrika ni miongoni mwa nchi zenye uchumi unaokua kwa kasi. Inakadiriwa kwamba kati ya mwaka 2012 mpaka 2017 katika nchi kumi zenye uchumi unaokua kwa kasi zaidi, sita zitakuwa zinatoka Bara la Afrika. Tanzania ni moja ya nchi hizo, nyingine ni Rwanda, Angola, Chad, Ethiopia na Equatorial Guinea.

Angola, Equatorial Guinea na Chad kasi yao ya kukuza uchumi inasukumwa na utajiri mkubwa wa mafuta na gesi. Hata hivyo, nchi hizi zipo chini katika viwango vya kidemokrasia na utajiri wa maliasili zao umekuwa ukinufaisha watu wachache. Kwa mfano, huko Angola na Equatorial Guinea, ni familia za marais wao (waliokaa madarakani kwa zaidi ya miongo mitatu) na familia za karibu na watawala ndizo zinanufaika na uchumi wa nchi zao. Hali ya ufukara wa wananchi katika nchi hizo hauwiani na mapato makubwa ambayo serikali zao zimekuwa zikipata kutoka katika mafuta na gesi asilia.

Nchini Rwanda, sekta ya huduma ndio inayoendesha uchumi ingawa mwaka jana wameweza kuvuka lengo la asilimia tano ya kasi ya kukua kwa sekta ya kilimo. Rwanda nao, licha ya mafanikio makubwa katika kutokomeza umasikini (theluthi ya wananchi wameondoka kwenye dimbwi la umasikini ndani ya miaka kumi, 2000 – 2010), bado kuna malalamiko makubwa ya utawala wa kiimla nchini humo.

Kwamba hakuna uhuru wa habari na Serikali ya Rais Paul Kagame inakandamiza sauti za upinzani. Je, mtawala wa imla mwenye kuleta ahueni kwa wananchi ni afadhali kuliko mtawala wa kidemokrasia mwenye kukuza umasikini? Hili ni swali ambalo wanazuoni wana majibu yanayotofautiana kwa kila hali.

Sekta ya Kilimo ikikua kwa kasi ya asilimia tano na kuendelea kwa miaka mitano mfululizo, inaweza kupunguza umasikini kwa zaidi ya asilimia 30 katika kipindi hicho. Ethiopia, kasi yake ya ukuaji wa uchumi inachochewa na sekta ya kilimo pamoja na sekta ya viwanda. Iwapo Ethiopia itaendelea na kasi ya ukuaji wa uchumi wa zaidi ya asilimia saba kwa mwaka, unaosukumwa na kilimo na viwanda, basi baada ya miaka 10 nchi hiyo itakuwa ‘power house’ ya Bara la Afrika.

Kama Rwanda, Ethiopia pia imeweza kutokomeza umasikini kwa kasi katika kipindi cha muongo mmoja uliopita, vile vile, kama Rwanda, uongozi wa Waziri Mkuu Meles Zenawi (sasa marehemu) umekuwa ukilalamikiwa kwa utawala wa kiimla licha ya mafanikio makubwa katika maendeleo ya kilimo na viwanda.

Tanzania haijaanza uzalishaji wa kiwango kikubwa wa rasilimali ya gesi na mafuta (ukiacha uzalishaji kidogo katika visima vya Songosongo), lakini sekta zinazoendesha ukuaji wa uchumi wake ni madini, mawasiliano na utalii. Kiwango cha umasikini nchini kimeshuka kutoka asilimia 37 mwaka 2003 mpaka asilimia 28 mwaka 2013. Kasi ya kutokomeza umasikini bado ni ndogo ukilinganisha na mataifa haya niliyoyataja hapo juu.

Midomoni mwa watawala wa Tanzania ni kwamba gesi asilia ndio mkombozi kwa sasa. Ngonjera hizo hizo zilikuwa zikiimbwa pale Tanzania ilipoingia kwenye uzalishaji mkubwa wa dhahabu. Wakati huo, Waziri wa sasa wa Nishati na Madini ndiye aliyekuwa Mwenyekiti wa Shirika la STAMICO ambalo liliachia migodi yake yote na kuwapa wawekezaji kutoka nje kwa nyimbo kwamba dhahabu itaondoa umasikini wetu. Miaka 17 sasa, ufukara wa wananchi upo pale pale na santuri imegeuzwa na sasa inaimba gesi asilia na Watanzania, wasomi na wasio wasomi wanacheza na kupiga makofi.

Nilimsikia Waziri wa Nishati na Madini akiwaeleza viongozi wa dini nchini mwanzoni mwa mwaka huu, mbele ya Rais Jakaya Kikwete kwamba; “tumelima wee, bado tu masikini. Tumefanya biashara, bado tu masikini. Sasa gesi imekuja, ndio mwarobaini wa umasikini”.

Nilitaraji Rais aliposimama kuzungumza angeweza kuweka maelezo sawia, lakini nadhani alishindwa kumsahihisha waziri wake mbele ya hadhara ile. Lakini pia inawezekana ndio msimamo wa serikali kuwapa matumaini wananchi kwamba ‘umasikini sasa basi’.

Gesi asilia hata igunduliwe kila kona ya nchi haitaweza kuondoa ufukara wa wananchi. Ingekuwa ni hivyo leo Nigeria ingekuwa taifa lenye watu wenye maendeleo kuliko mataifa mengi duniani. Lakini Nigeria bado, licha ya kuwa na uchumi mkubwa zaidi Afrika, ina watu mafukara wa kutupwa.

Pato la mwananchi wa Nigeria ni chini ya dola za Marekani 1,500 kwa mwaka, yaani ni nusu tu ya nchi kama Mauritius isiyo na chembe ya mafuta. Mifano ya Angola, Equatorial Guinea na Gabon inatosha kabisa kuwakumbusha watawala wetu kwamba mafuta au gesi asilia ni mwarobaini wa umasikini.

Nchi zote hizi hazijafanikiwa kwa sababu ya ufisadi mkubwa unaotokana na usiri katika mikataba ya madini, mafuta na gesi asilia. Hapa Tanzania mikataba yote hiyo bado ni siri na matokeo yake ni upotevu mkubwa wa fedha tunaotarajia kushuhudia kutokana na mikataba mibovu.

Tayari mkataba uliovuja wa kampuni ya StatOil umeonyesha kuwa Tanzania itapoteza shilingi trilioni moja na bilioni 600 kila mwaka kwa miaka 15, katika kitalu kimoja tu (block 2). Hatujui mikataba mingine 26 hali ikoje maana yenyewe haijavuja.

Mwarobaini wa umasikini ni kazi
Tanzania imejaribu kila aina ya mipango ya maendeleo. Miaka takribani 25 ya mwanzo wa Uhuru wetu tumeitumia kujenga taifa la kijamaa. Katika mapumziko yangu ya mwisho wa wiki, wiki hii iliyokwisha nilikuwa nasoma uchambuzi kuhusu utekelezaji wa vijiji vya ujamaa. Katika kitabu kimoja cha Andrew Coulson (Political Economy of Tanzania) ameainisha namna Dola ilivyoamua kusukuma yenyewe maendeleo.

Mmoja wa vijana wa wakati huo, Juma Mwapachu (sasa balozi mstaafu) alinukuliwa akiandika; “Nchi haiwezi kuacha raia wake wakiishi maisha ya kifo – life of death. Jioni ya Jumamosi nilikutana na Balozi Mwapachu nikamuuliza, unaweza kuandika tena vile? Akasema kwa ujasiri kabisa, “ndio mwanangu.”

Dola ilidhamiria kweli kweli. Dola iliamini kwa dhati kabisa kwamba inalo jukumu la kuchochea maendeleo. Utekelezaji wa ujamaa uliendana na makosa mengi ya uharibifu wa mali na hata ukiukwaji wa haki za binadamu. Lakini dhamira ilikuwa kazi– kuongeza tija kwenye uzalishaji mali, viwandani na mashambani.

Miaka 25 iliyofuatia Tanzania ikahamia kutekeleza sera za soko huria na kuitoa dola kwenye kusukuma maendeleo ya watu wake. Bahati mbaya, soko huria likawa soko holela kutokana na kukosekana mipango ya kidola ya kusawazisha makosa ya soko.

Nimebahatika kushiriki katika baraza kubwa zaidi nchini, Bunge, tena nikiwa Mwenyekiti wa Kamati inayotazama matumizi yetu (postmorterm) kwa miaka yote isipokuwa miwili ya mwanzo. Nimebahatika kuwa kiongozi mwandamizi katika chama kimojawapo kikuu cha siasa nchini.

Nafasi zote hizo nimezishika nikiwa kijana mdogo. Sijaona ushahidi wowote kwamba taifa lilijiandaa kutoka mfumo wa uchumi wa kijamaa kwenda uchumi wa soko huria. Ndani ya Bunge na ndani ya vikao vya vyama vya siasa hakuna mijadala inayohusu maendeleo ya watu, zaidi ya namna gani ya kuendelea kushika dola au namna gani ya kupata dola.

Ndio maana tunashuhudia kwenye mikutano ya vyama na hasa nyakati za uchaguzi wanasiasa wakihubiri mrengo mmoja wa maendeleo (soko huria) na kushindanisha orodha ya miradi badala ya kushindanisha maono (visions) na itikadi za kimaendeleo.

Ninapojisomea zaidi naona kama tulikurupuka, tukaachana na ujamaa na mazuri yake na mabaya yake na kukumbatia ubepari bila kuchukua hadhari kuhusu mabaya yake. Wale wale waliokuwa wanahubiri ujamaa ndio wakaanza kuhubiri uzuri wa soko huria.

Ngonjera zilezile, matokeo yake ni umasikini kuongezeka maradufu, tofauti ya walio nacho na wasionacho kuendelea kupanuka. Tulipotupilia mbali dhana ya uzalishaji mali mashambani na viwandani, tukakumbatia uchuuzi. Sasa tumekuwa taifa la wachuuzi. Uchuuzi hauzalishi kazi nyingi na pasipo na kazi ufukara hushamiri.

Mipango ipi inafaa kutuondoa katika dimbwi la ufukara? Kamwe tusidhani utajiri wa gesi asilia utatutoa. Utajiri huu utaongeza pengo la wenye nacho na wasio nacho kwa sababu mipango ya sasa ya uchumi imewekwa kwenye nguzo ya mwenye nguvu ndiye anafaidika.

Nguvu inatokana na taarifa (information is power) na taarifa kwa nchi kama yetu zinazaa vipato nyemelezi (rent seeking) ambazo zinanufaisha wachache. Ndivyo imetokea kwenye sekta ya madini na mawasiliano, ambapo wenye taarifa ndio wamefaidika na wananchi wengi na hasa vijana wamebakia wapagazi wa wenye taarifa (rent seekers).

Hawa kina Mwapachu, vijana wa zamani, walikuwa wanaimbishwa kuwa kazi ni kipimo cha utu. Mipango ya kutuondoa kwenye ufukara ni mipango ambayo imejikita kwenye nguzo zinazozalisha kazi na maarifa ya kufanya kazi.

Kwa sasa kazi ambazo zitanufaisha Watanzania wengi ni kazi za kilimo. Kilimo sio kazi ya shambani tu, ni pamoja na mnyororo wake wa thamani (value chain). Sera ya ujamaa ilijenga viwanda vya kuongeza thamani mazao ya kilimo. Kulikuwa kuna kiwanda cha nguo katika kila kanda ya Tanzania na kiwanda kikubwa cha nyuzi Tabora bila kutaja ginneries (vinu vya uchambuaji) zilizozagaa vijijini.

Sera ya ujamaa ilijenga viwanda vya kubangua korosho 12 katika wilaya zote zinazozalisha zao hilo. Sera yetu mpya ya nusu ya pili ya miaka ya Uhuru imefanya nini? ‘deindustrialisation’ kwa jina la ubinafsishaji.

Nilikwenda kukagua viwanda vya korosho mwaka 2012, kama Mwenyekiti wa Kamati ya Posmortem (PAC), nilikuta viwanda vyote vimegeuzwa kuwa maghala ya kuhifadhi korosho. Nilikwenda mji mdogo wa Choma huko Igunga- mkoani Tabora, nilikuta iliyokuwa ginnery (kiwanda cha kuchambua pamba) kimetelekezwa na mwekezaji.

Korosho yetu yote tunayouza nje hivi sasa ni korosho ghafi, tunahamishia ajira India tunapouza korosho yetu nyingi. Tunauza marobota ya pamba na kuagiza mashati na suruali tunazovaa na kujidai mitaani. Hakika hakuna umazwazwa (ujuha) zaidi ya huu. Hebu tujadili, ujamaa ulikosea wapi? Mbona sera hizi mpya ndizo zinatutia ufukara zaidi?

Nilisoma nikiwa darasa la nne, ‘kama unataka mali, utayapata shambani’. Ujamaa ulitaka kazi. Waliotekeleza Azimio la Arusha hawakutaka kazi, fursa ilipofika wakatupilia mbali Azimio. Lakini bado nchi ipo pale pale au imekuwa mbaya zaidi. Turudi kwenye misingi. Hakuna namna! Tuutafakari kwa kina na kwa kukosoa ujamaa. Tutafakari kwa kina na kukosoa sera za sasa. Kisha tuunde kitu kipya. Miaka 50 inatosha kutakafakari majaribio yetu.

– See more at: http://www.raiamwema.co.tz/gesi-si-mwarobaini-wa-umasikini-kazi-shambani#sthash.X1qbO5iU.Mw88XujN.dpuf