Gama awataka wakuu wa idara kuacha ‘uvivu’

Halmashauri ya Manispaa ya Moshi

Na Mwandishi Wetu, Moshi

WAKUU wa idara wilaya na kata mkoani Kilimanjaro, wametakiwa kutoka ofisini na kwenda vijijini kufanya kazi na wananchi, hatua ambayo itasaidia kupunguza kero zilizopo.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama, wakati akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Sungu kata ya Kibosho mashariki wilaya ya Moshi, ambapo alisema kumekuwepo na migogoro mingi katika jamii ambayo mingi imekuwa ikisababishwa na watendaji kutowajibika kikamilifu.

Gama alisema wapo watumishi ambao toka wameteuliwa na serikali hawajawahi kufika vijijini kukutana na wananchji na badala yake wamekuwa wakikaa maofisini jambo ambalo amesema hawezi kulifumbia macho na kuliacha liendelee.

Alisema wajibu wa watumishi ni kufanya kazi na wananchi vijijini na mkuu wa idara hana sababu ya kukaa ofisini kwa kisingizio cha kukosa fedha za kwenda vijijini kutokana na kwamba ameajiriwa na serikali kwa ajili ya kufanya kazi hivyo kama nikwenda kwa wananchi kinachohitajika ni usafiri na sikitu kingine.

“Tumekuwa na changamoto kubwa sana ya wataalamu kukaa maofisini, hili ni tatizo kubwa kwani serikali imeajiri wataalamu kwa ajili ya kuwasaidia wananchi lakini cha ajabu wataalamu hawa wamejilundika katika halmashauri huku wananchi wakishindwa kusonga mbele kimaendeleo kwa kukosa wataalamu wa kuwaelekeza, sasa nawataka kwenda vijijini kutoa ushauri wa kitaalamu kwa wananchi,” alisema Gama.

Alisema serikali imekuwa ikilaumiwa sana na wananchi lakini tatizo kubwa liko kwa watendaji ambao wamekuwa wakishindwa kutekeleza majukumu yao ipasavypo, na kuishia kukaa maofisini kwa kisingizio kuwa hawana posho za kwenda vijijini ili hali wameajiriwa na serikali kufanya kazi kuanzia saa Moja na nusu asubuhi hadi saa Tisa na nusu alasiri i na mshahara wanapata.

Katika hatua nyingine Mkuu huyo aliwataka wakuu wa wilaya kuwa na vikao na wakuu wa idara kila mwezi na katika vikao hivyo kila mkuu wa idara aelezi ni nini ambacho amekifanya katika mwezi huo hatua ambayo itasaidia kukomesha tabia ya watumishi kukaa maofisini.

Aliitaka pia kamati ya maendeleo ya kata kila inapokutana kuhakikisha agenda ya kwanza inakuwa ni kila mkuu wa idara katika kata kueleza amefanya nini katika kipindi cha miezi mitatu ndipo agenda nyingine ziendelee na kwamba kwa kufanya hivyo kutasaidia kuondoa uzembe uliojengeka kwa watendaji wengi ndani ya kata na hata halmashauri.

Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama yuko katika ziara wilaya ya Moshi kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo, ambapo pamoja na kukutana na wananchi mkuu huyo pia alikagua ujenzi wa Bwalo la shule ya sekondari ya Mangi sabas, Kuona ujenzi wa Bweni Sungu Sekondari pamoja na kitalu cha miti kwa Sebastian Chuwa.