Na Mwandishi Wetu, Arusha
MWENYEKITI wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe leo amefikishwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Arusha na kuunganishwa katika kesi inayomkabili Katibu Mkuu wa Chama hicho Dk. wilbroad Slaa na Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki Tundu Lissu na wenzao 25 ambapo anakabiliwa na mashitaka mawili.
Mwendesha Mashitaka wa Serikali Haruna Matagane aliieleza mahakam hiyo mbele ya hakimu Devotha Kamuzora, kosa la kwanza linalomkabili Mbowe ni kufanya kusanyiko haramu lisilokuwa na kibali kinyume cha kifungu cha sheria 74 (1) na kifungu cha sheria cha 75 cha Jeshi la Polisi, mnamo Novemba 7 mwaka huu majira ya usiku hadi Novemba 8 majira ya saa 12 asubuhi katika uwanja wa NMC Manispaa ya Arusha.
Katika shauri hilo lenye namba 454 la mwaka 2011, Matagane alidai kuwa shitaka la pili linalomkabili Mwenyekiti huyo ni kutotii amri halali
ya Jeshi la Polisi mkoani Arusha lililotolewa na Mkuu wa Operesheni
maalumu mkoani hapa, Peter Mvulla ambaye, amri ililowataka kutawanyika katika uwanja huo.
Naye Wakili wa utetezi Method Kimomogolo aliiomba mahakama hiyo
kumpatia mshtakwia huyo dhamana kwa masharti waliyokuwa wamepwa
wenzake. Hakimu Kamuzora alikubaliana na maombi hayo na kutoa masharti ya dhamana kam waliyokuwa wamepewa watuhumiwa wenzake Mbowe ikiwa ni wadhamini wawili kwa ahadi ya sh. milioni 5 kila mmoja. Kwa upande wake wakili wa Serikali aliiomba mahakama hiyo kuahirisha shauri hilo kutokana na upelelezi wa kutokukamilika.
Baada ya kusomewa mashitaka hayo Mbowe alikana na mashitaka hayo na Hakimu kuahirisha shauri hilo hadi Novemba 22 mwaka huu kwa ajili ya kutajwa ambapo ataungana na washitakiwa wengine 27. Awali Dk. Slaa na wenzake 26 waliburuzwa mahakamani hapo Novemba 8 mwaka huu, ambapo Mbowe alitakiwa kujisalimisha Polisi baada ya kuwakimbia polisi wakati walipokuwa wanatawanywa katika uwanja wa NMC Novemba 7, ili aweze kuunganishwa katika shauri hilo.
Aidha Mbowe juzi baada ya kuhojiwa, alitakiwa kuripoti kituoni hapo
jana ambapo alifika majira ya saa 3;36 baada ya polisi juzi kumkatalia
madai yake ya kutaka kulala kituoni hapo hadi jana atakapofikishwa
mahakamani.
Mwenyekiti huyo juzi baada ya kuhojiwa na kufanya mazungumzo
na DCI Robert Manumba, Mkuu wa operesheni maluum wa jeshi la polisi
Simon Sirro, Kamishna wa Operesheni na mafunzi nchini Paul Chagonja na Mkuu wa intelijensia Hussein Laizer, aliwaeleza waandishi wa habari leo kuwa alilazimika kuwapigia simu viongozi wa Chadema ngazi za wilaya na mikoa kote nchini kusitisha maandamano yaliyokuwa yamepangwa kufanyika.
Alisema kuwa katika majadiliano baina yake na maofisa hao wa ngazi za
juu wa Polisi, walikubaliana kufanya mazungumzo ili kuweza kubaini
tatizo la migogoro inayojitokeza baina ya Jeshi hilo na CHADEMA.
Aidha alisema kuwa katika mazungumzo hayo pia kutatafutwa chanzo cha tatizo la Arusha ili kuweza kulitafutia muafaka na kuondoa mvutano
ambao umekuwa kwa kipindi cha mwaka mmoja sasa.