VITA ya kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 imeingia katika sura mpya baada ya Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye kumlalamikia mrithi wake katika wadhifa huo, Edward Lowassa akimtuhumu kumfanyia mbinu chafu.
Huku akinukuu habari iliyoandikwa na gazeti hili Septemba 16, 2013 yenye kichwa cha habari, ‘Lowassa afichua siri ya mradi wa maji Ziwa Victoria’, Sumaye alisema Lowassa amekuwa akimfanyia propaganda na mbinu chafu.
Katika habari hiyo, ambayo Lowassa alialikwa katika Harambee ya kuchangia Shule ya Msingi ya Kanisa la AICT huko Kahama, Shinyanga hivi karibuni, alikaririwa akisema mawaziri watatu, tu ndiyo waliounga mkono wakati alipopendekeza kutekelezwa kwa mradi huo kwenye kikao cha Baraza la Mawaziri cha Serikali ya Awamu ya Tatu iliyokuwa chini ya Benjamin Mkapa.
Lowassa, ambaye katika kipindi hicho alikuwa Waziri wa Maji na Maendeleo ya Mifugo, aliwataja mawaziri waliounga mkono mradi huo kuwa ni Rais Jakaya Kikwete ambaye wakati huo alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Mohamed Seif Khatibu, aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Sumaye
Alisema hizo ni mbinu chafu zilizokuwa na lengo la kumpaka matope… “Najua mhusika ametumia sana mradi huu kisiasa na sisi wengine tumenyamaza japo ukweli tunaujua. Amenilazimisha niseme ukweli kuhusu mradi huu kwa sababu mimi nilikuwa Waziri Mkuu na mradi umetekelezwa chini ya uangalizi wangu,” alisema na kuongeza:
“Kama Waziri anaweza kubuni na kutekeleza mradi mkubwa hivyo peke yake, akiwa Waziri Mkuu si maji yangefika Dodoma? Mbona hata bado kuna kuna sehemu za Kanda ya Ziwa bado kuna shida ya maji?” alihoji Sumaye, ambaye alikuwa Waziri Mkuu kwa miaka 10 katika Serikali ya Awamu ya Tatu.
Alipotafutwa kwa simu kuelezea madai hayo, Lowassa, ambaye yuko Dodoma akihudhuria vikao vya Bunge, alisema hawezi kubishana na Sumaye kwa kuwa anamheshimu kwani amewahi kuwa kiongozi mkubwa serikalini.
“No comment’ (sina la kusema), siwezi kubishana na Sumaye kwani amewahi kushika nyadhifa za juu katika nchi hii,” alisema Lowassa, ambaye pia ni Mbunge wa Monduli (CCM).
Sumaye alimtuhumu Lowassa kwa kusema uongo na kuongeza kuwa amefanya kosa la jinai kutoa siri za Baraza la Mawaziri.
“Pamoja na kwamba hilo lililoelezwa ni uongo mkavu, mhusika kama waziri mwandamizi wakati huo na sasa anawinda nafasi kubwa katika nchi, hakutegemewa kutoa siri za Baraza la Mawaziri, labda amediriki kufanya hivyo kwa sababu anajua anayosema siyo ya kweli, vinginevyo ni kosa la jinai na akishtakiwa anafungwa jela,” alisema.
Sumaye alisema hizo ni mbinu chafu zinazofanywa dhidi yake kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
“Ziko mbinu nzuri na za kistaarabu na ziko mbinu chafu kama za kupakana matope (character assassinations). Mtu wa kwanza anajisafishia njia yake kwa kufyeka miiba na kuondoa magogo njiani ili wakati ukiwadia, mbio zake zisikwazwe na vigingi vyovyote. Aina ya pili ya mbinu chafu ni pale mhusika anapotengeneza mbinu za kuwamaliza wengine wanaodhaniwa kuwa washindani wake,” alisema Sumaye.
Hata hivyo, alipoulizwa kama amejipanga kugombea urais mwaka 2015, Sumaye alisita kujibu kwa muda mrefu, lakini baadaye akajibu:
“Nasema hivi, kama ni kugombea nina haki zote, kama ni uwezo ninao, kama ni imani ya Watanzania kwa sehemu kubwa ninayo. Kilichobaki ni uamuzi tu wa mimi kutamka. Kwa hiyo sijatamka msije mkasema nagombea urais. Nasema tu na mimi katika Watanzania wanaofikiriwa na mimi nasikia nimo. Kwani ninyi hamnifikirii? Sasa itakapofika huko mbele, si tutaamua wakati huo?”
Kuhusu hujuma zinazofanywa katika shughuli za jamii kwa maslahi ya siasa, Sumaye alisema kuna watu wanaomfanyia hujuma na kuzuia mialiko yake. Alitoa mfano wa mwaliko wa Oktoba 27 mwaka huu wa kupokea maandamano ya kikundi cha Joggers katika shughuli, ambayo ilikuwa ifanyike Mnazi Mmoja, Dar es Salaam.
“Dakika za mwisho nikapewa taarifa kuwa shughuli imeshindikana kwa sababu imeingiliwa na kikundi chenye kulinda masilahi yake au ya mtu wao. Shughuli hiyo baadaye ilifanyika na kupatikana ‘mgeni rasmi’ mwingine,” alisema.
Hata hivyo, katika hatua nyingine, Shirika la Faita Jogging Sports Clubs limekanusha kumwalika Sumaye kwenye shughuli yao ya Mnazi Mmoja.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mwenyekiti wa shirika hilo, Steven Kaema alisema shirika hilo halikufanya mawasiliano ya aina yoyote na Sumaye tofauti na anavyodai.
“Hatukuwa na mawasiliano yoyote na Sumaye, sisi tulituma barua ya mwaliko kwa Makamu wa Rais ambaye alitujibu kuwa hatakuwepo siku hiyo na tulituma barua nyingine kwa Naibu Waziri wa Elimu, Philipo Mulugo ambaye naye alijibu kuwa atasafiri kwa hiyo ofisi yetu haina barua yoyote ya kumuomba Sumaye kuwa mgeni rasmi,” alisema Kaema.
“Mara ya pili ni mwaliko wa kuzindua Saccos ya Nshamba Muleba, Kagera, Oktoba 28,” aliendelea Sumaye… “Mwaliko huu sikuomba, bali viongozi wa chama walinipendekeza kwa sababu zao wenyewe. Wakati najiandaa kwenda, nikaambiwa shughuli zimeingiliwa na watu fulani kwa kutoa rushwa kwa baadhi ya viongozi wa Saccos.”
Alipotakiwa kuwataja watu hao anaodai kuwa wanamhujumu, Sumaye katika mialiko yake, alijibu:
“Siwataji, hata ninyi mnawajua. Nataka niwataaarifu hao wanaohangaika na mialiko yangu kwa taarifa yao ninayo mingi mpaka mingine nakosa muda wa kuhudhuria. Siitwi kwa sababu ya fedha maana wanajua sina fedha za aina hiyo maana sijaiibia nchi na watu wake,” alisema Sumaye.
Alidai kuwa wanaomhujumu wanafanya hivyo ili kumzima asizungumzie rushwa, ufisadi na dawa za kulevya… “Fisadi huliibia taifa fedha nyingi kiasi cha wananchi kutaabika halafu huja kutoa kijisehemu cha fedha alizofisadi kwa njia ya rushwa kukandamiza maendeleo ya watu.”
Rushwa CCM
Sumaye alimpongeza Rais Jakaya Kikwete kwa kupambana na rushwa na kutahadharisha kuwa tatizo hilo linaweza kukiangusha chama hicho. Aliahidi kuwa na Rais bega kwa bega katika vita hiyo.
“Rais Kikwete amesema kuwa rushwa inaweza ikafanya chama hiki kikashindwa. Mimi naamini, kama CCM itapitisha majina kwa kuangalia rushwa bila kujali, chama kitaanguka, bahati nzuri Mwenyekiti ameliona hilo, siamini kama watapitisha watu ambao watakiangusha… waliopitishwa kama hawataenguliwa, sitaweza kukaa nao, hata kama sitahama.”
CHANZO: Gazeti Mwananchi