UONGOZI wa waandaaji wa Tamasha la Kimataifa la Filamu za Nchi za Jahazi (ZIFF), mapema leo Mei 19.2017, wametangaza rasmi filamu zilizochaguliwa kwa mwaka huu na ambazo zitaoneshwa kwenye tamasha hilo msimu wa 20, hapo Julai 8-16-2017. Akizungumza na waandishi wa Habari Jijii Dar e Salaam, Mkurugenzi wa ZIFF, Bw. Fabrizio Colombo amesema kuwa, jumla ya filamu 132, zimeweza kuchaguliwa kuingia kwenye tamasha hilo.
“Jumla ya filamu 600,zilitumwa kwetu ZIFF kutoka nchi 70, Duniani kote. Lakini katika hizo, filamu 132 ndizo tulizozichagua na zitapata kuoneshwa kwa mwaka huu pale Ngome Kongwe, Zanzibar.
Katika filamu hizo 132, filamu 23 zinatoka Tanzania. Lakini pia zikiwa zimegawanyika katika aina mbalimbbali ikiwemo filamu ndefu, filamu fupi, filamu za katuni, na filamu zingine nyingi huku pia mwaka huu tumepata filamu kutoka nchini Namibia” ameeleza Mkurugenzi huyo Colombo. Kwa upande wake Meneja wa ZIFF, Daniel Nyalusi amebainisha kuwa, katika filamu hizo 23 kutoka Tanzania zimeweza kukidhi vigezo hivyo kuoneshwa kwake ZIFF mwaka huu zitaongeza ufanisi na soko la filamu za Tanzania licha ya kuwa na changamoto nyingi ikiwemo kukosa soko la ndani kutokana na na nyingi kuandaliwa kwa bajeti ndogo, kukosa ubunifu katika uandishi wa stori na mengine mengi.
“Soko la filamu linakua na zinaanza kuwa nzuri, lakini wingi wa uzalishaji umepungua. Ukosefu wa bajeti unapelekea wataarishaji kushindwa kutengeneza filamu zenye ubora na viwango vya kimataifa. Pia ukosefu wa ubunifu wakati wa uandishi wa stori nako pia kuna sababisha filamu zetu kukosa ubora,” amesema na kuongeza.
“Watunzi wetu wanaona lazima watunge stori zinazohusu mapenzi ndio zitanunulika, inabidi wabadilike namna ya uandishi pia tukubali kuongeza elimu na kuzitengeza filamu kulingana na bajeti iliyopo. Angalie filamu ya Kiumeni, ni ya bongo movie lakini ina stori tofauti sababu ya ubunifu wa hali ya juu uliotumika.”
Amesema ili kuondoa ukata wa fedha za kutengenezea filamu zilizo bora, wasanii inabidi wawashawishi wadhamini mbalimbali kudhamini filamu zao kama zinavyofanya nchi zilizoendelea.
“Kwenye filamu unakuta msanii anakunywa bia ya safari, anaitangaza ila watengenezaji bia hiyo hawawalipi. Lakini nchi za wenzetu wasanii wanatumia filamu kutangaza bidhaa zao. Lazima wakubalia kuanza tabia ya kushawishi wadhamini katika filamu zetu,” amesema.
Tamasha la ZIFF mwaka huu 2017, ni la 20, tokea kuanzishwa kwake na ufanyika kila mwaka katika viunga vya Ngome Kongwe, Unguja ambapo limekuwa likiwakutanisha watu mbalimbali kutoka pembe za Ulimwengu wakijumuika pamoja na kushuhudia filamu mbalimbali zikioneshwa sambamba na uwepo wa Makongamano, Warsha, biashara, mafunzo kwa Jamii, Pia uwepo majukwaa ya Watoto, Wanawake (Panorama) pamoja na Muziki kutoka kwa vikundi na bendi mbalimbali za ndani na nje.