FIFA yaipandisha Tanzania kiwango cha soka

Bendera ya Tanzania

Tanzania imepanda kwa nafasi 12 kwenye orodha ya viwango vya ubora ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) iliyotolewa leo Julai 4 mwaka huu na shirikisho hilo.

Kwa viwango vya Juni mwaka huu, Tanzania (Taifa Stars) ambayo timu yake inadhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager ilikuwa namba 139 hivi sasa imefika nafasi ya 127 ikiwa na pointi 253 kulinganisha na 214 za Juni mwaka huu.

Ivory Coast inayoshika nafasi ya 16 duniani bado inaongoza kwa upande wa Afrika ikiwa na pointi 939. Timu hiyo ilikuwa katika nafasi hiyo hiyo kwa viwango vilivyotolewa Juni 6 mwaka huu. Hispania ambao ni mabingwa wa Ulaya na Dunia ndiyo wanaoendelea kuongoza kwa kukamata nafasi ya kwanza wakiwa na pointi 1,691.