FIFA Yaipa TFF Tiketi 260 za Kombe la Duniam, AFCON Kupangwa..!

FIFA Yaipa TFF Tiketi 260 za Kombe la Dunia

FIFA Yaipa TFF Tiketi 260 za Kombe la Dunia

SHIRIKISHO la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) limeipa Tanzania mgawo wa tiketi 260 za Fainali za Kombe la Dunia nchini Brazil. Watanzania wanaohitaji tiketi hizo wanatakiwa kutuma maombi TFF kwa maandishi wakielezea aina ya tiketi na mechi wanazotaka kushuhudia. Hakuna tiketi zitakazoombwa FIFA bila kuwepo maombi kwa maandishi.
 
Tiketi zilizopo kwa Tanzania ni ifuatavyo; kwa hatua ya makundi (ukiondoa mechi ya ufunguzi), raundi ya 16 bora, robo fainali na mechi ya kutafuta mshindi wa tatu ni 250.
 
Kwa mechi ya ufunguzi, nusu fainali mbili na fainali (mechi namba 1, 61, 52 na 64) ni tiketi kumi tu ndizo zitakazopatikana. Bei za tiketi ziko katika viwango vitatu tofauti.
 
Mechi ya ufunguzi tiketi zake ni dola za Marekani 495, 330 na 220. Hatua ya makundi (mechi namba 2-48) ni dola 175, 135 na 90. Hatua ya 16 bora (mechi namba 49-56) ni dola 220, 165 na 110.
 
Robo fainali (mechi namba 57-60) ni dola 330, 220 na 165 wakati nusu fainali (mechi namba 61 na 62) ni dola 660, 440 na 275. Mechi ya mshindi wa tatu ni dola 330, 220 na 165. Kiingilio kwa fainali kitakuwa dola 990, 660 na 440.
 
TFF itawasilisha maombi ya tiketi hizo FIFA kuanzia Desemba 8 mwaka huu  hadi Februari 7 mwakani. Idadi ambayo itaombwa FIFA itatokana na Watanzania waliowasilisha maombi TFF kwa vile zinaweza zisipatikane tiketi zote hizo zilitengwa kwa Tanzania. Hivyo tunasisitiza maombi ya tiketi yatakayofanyiwa kazi ni yale ambayo yamewasilishwa TFF kwa maandishi tu.
 
JOPO LA WATAALAMU KUPANGA MKAKATI WA AFCON 2015
Jopo la wataalamu 20 walioteuliwa na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi linakutana kupanga mkakati wa kuonesha jinsi Tanzania inavyoweza kushiriki Fainali za Afrika (AFCON) zitakazofanyika mwaka 2015 nchini Morocco.
 
Kikao hicho maalumu (retreat) kitafanyika mjini Zanzibar kuanzia Desemba 6-8 mwaka huu. Jopo hilo litaongozwa na Mwenyekiti wa zamani wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Kanali mstaafu Idd Omari Kipingu.
 
Wengine wanaounda jopo hilo linalohusisha pia makocha ni Dk. Mshindo Msolla, Peter Mhina, Ayoub Nyenzi, Abdallah Kibaden, Pelegrinius Rutahyuga, Kidao Wilfred, Salum Madadi, Juma Mwambusi, Ken Mwaisabula, Boniface Mkwasa, Fred Minziro, Meja Abdul Mingange, Ally Mayay, Boniface Mkwasa na Dan Korosso. Wajumbe wengine wa jopo hilo wanatoka Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA).
 
*Imeandaliwa na Boniface Wambura Mgoyo, Kaimu Katibu Mkuu
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)