FIFA kutoa kozi kwa waamuzi Dar es Salaam

Logo ya Chama cha Soka Ulimwenguni (FIFA)

KOZI ya wakufunzi wa waamuzi (Futuro III Refereeing Course) ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) inaanza Septemba 10 mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Jumla ya washiriki katika kozi hiyo itakayoanza saa 3 asubuhi kwenye hoteli ya Holiday Inn ambao wanatoka katika nchi 21 za Afrika ni 69. Kozi hiyo inayotarajiwa kumalizika Septemba 22 mwaka huu inafanyika katika maeneo mawili ya ufundi (technical) na utimamu wa mwili (fitness).

Nchi washiriki ni Afrika Kusini, Botswana, Eritrea, Ethiopia, Gambia, Ghana, Kenya, Lesotho, Liberia, Malawi, Mauritius, Namibia, Nigeria, Seychelles, Sierra Leone, Somalia, Swaziland, Tanzania, Uganda, Zambia na Zimbabwe.

Washiriki kutoka Tanzania kwenye kozi hiyo ni Joan Minja, Leslie Liunda na Soud Abdi (technical) na Riziki Majalla (fitness).

Baadhi ya wakufunzi wa kozi hiyo wanaotoka FIFA na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) ni Carlos Henriques anatoka Afrika Kusini, Fernando Gracia (Hispania), Steve Bennett (Uingereza), Tarek Bouchamaoui (Tunisia), James Sekajugo (Uganda), Bester Kalombo (Malawi), Felix Tangawarima (Zimbabwe) na An-Yan Lim Kee Chong (Mauritius).

Kozi hiyo itafunguliwa na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya CAF na mjumbe wa Kamati ya Vyama (Associations Committee) ya FIFA.

Wakati huo huo; Timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 (Serengeti Boys) inaendelea vizuri na kambi ya mazoezi mkoani Mbeya ambapo tayari imecheza mechi moja ya kujipima nguvu.

Ilicheza mechi hiyo Septemba 8 mwaka huu dhidi ya Tanzania Prisons iliyoko Ligi Kuu ya Vodacom kwenye mji wa Nakonde ulioko mpakani mwa Tanzania na Zambia. Timu hizo zilitoka sare ya 1-1 huku bao la Serengeti Boys likifungwa na Miraji Selemani.

Serengeti Boys Septemba 9 mwaka huu imecheza mechi nyingine wilayani Mbozi dhidi ya Mbozi United. Itacheza mechi ya tatu Septemba 11 mwaka huu jijini Mbeya dhidi ya timu ya daraja la kwanza ya Mbeya City.

Kwa mujibu wa Kocha wa timu hiyo, Jakob Michelsen kambi hiyo inaendelea vizuri, na anatarajia kupata mechi moja ya kirafiki ya kimataifa kabla ya kucheza mechi ya mashindano na Misri, Oktoba 13 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.