RAIS wa shirikisho la soka Ulaya, UEFA Michel Platini anasema FIFA lazima kuimarisha sifa nzuri ulimwenguni
Michel Platini, na wakauu wengine saba kutoka barani Ulaya, watafanya kwanza mkutano wao kando ili kukubaliana katika mambo machache ambayo wangelipenda kutiliwa maanani na Sepp Blatter, na raia wa Ufaransa Plattini anasisitiza juu ya kupitisha mapendekezo hayo ambayo yataipatia nguvu mamlaka zaidi kamati ya maadili ili kupambana na visa vya ufisadi.
Blatter tayari ametangaza mipango kadha ya mabadiliko, ikiwa ni pamoja na kuyaruhusu mataifa yote 206 wanachama FIFA, kuamua nchi ambazo zitaweza kuandaa fainali za Kombe la Dunia miaka ijayo, kinyume na ilivyokuwa zamani, uamuzi ukifanywa na kamati kuu ya wanachama 25.
Makamu rais wa FIFA, Jim Boyce, anahisi kwamba kikao cha leo, na ambacho kitakwisha Ijumaa, ni fursa muhimu kwa FIFA kuweza tena kuimarisha sifa zake kama ilivyokuwa zamani, kufuatia shirikisho kugubikwa na visa vingi vya ufisadi katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.
Maafisa wawili wakuu walipigwa marufuku mwaka jana kushiriki katika shughuli za soka kufuatia uchunguzi uliofanywa na gazeti la Uingereza la Sunday Times, na mwaka huu, Mohamed Bin Hammam, aliyetaka kugombea kiti cha urais wa FIFA, alipigwa marufuku katika maisha yake yote asijiingize katika soka kufuatia madai ya hongo pia.
Boyce, kutoka Ireland ya Kaskazini, na ambaye alichukua madaraka kutoka kwa Geoff Thompson, kutoka England, mwezi Juni, alisea; “Hii itakuwa ni mara yangu ya kwanza kuhudhuria kikao kikuu cha FIFA, na ni matazamio yangu ni kwamba rais wa FIFA ataweza kutangaza baadhi ya mapendekezo ambayo tayari ameanza kuyatekeleza”.
“Ninaamini kwamba wajumbe wote wa Ulaya watakuwa na mapendekezo sawa na yangu. Wanachama wa Ulaya wa FIFA niliozungumza nao, na kamati kuu ya UEFA, wote wana mtizamo sawa ya jinsi tunavyotaka FIFA kusonga mbele.”
-BBC