SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu duniani (FIFA) limeahidi kuboresha makao makuu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) yaliyoko kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Ilala ili yawe katika kiwango cha kisasa ikiwa ni pamoja na kuwa na vitendea kazi na miundombinu ikiwa ni pamoja na upanuzi wa ofisi. Hatua hiyo itaiwezesha TFF kuwa na mazingira bora ya kufanya shughuli zake kwa ufanisi.
Vilevile kupitia programu zake mbalimbali ikiwemo ile ya Goal, FIFA imeahidi kushirikiana na TFF katika kuendeleza mradi wa kiuchumi kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume. Mwanzoni mwa mwaka huu, TFF ilihamishia makao yake makuu katikati ya jiji ili kupisha maendeleo ya kuiwezesha Karume kuwa kituo cha kisasa kwa michezo na vitega uchumi.
Akiongea mwishoni mwa ziara ya kikazi nchini, Meneja Miradi wa FIFA anayeshughulikia Programu za Afrika, Zelkifli Ngoufonja amesema FIFA inaunga mkono wazo la kuboresha makao makuu ya Karume na itasaidia kwa awamu uboreshaji huo.
Katika kuhakikisha usimamizi na utekelezaji barabara wa mradi huo, ujumbe huo wa FIFA ulikubaliana na Kamati ya Utendaji ya TFF kuboresha ofisi za Karume ili jengo la utawala lianze kutumika huku mradi ukitekelezwa kwa awamu.
Pamoja na kuongelea mradi huo muhimu kimichezo na kibiashara, ujumbe huo uliokuwa nchini kwa juma moja kufuatia mwaliko wa TFF ulikuwa na nafasi ya kujadiliana na TFF kuhusu maboresho katika masuala mbalimbali yakiwemo ya Utawala, Fedha, Masoko, Ufundi, Mashindano na timu za taifa.
Akiongea kwa niaba ya Kamati ya Utendaji ya TFF, Rais wa TFF Jamal Malinzi aliushukuru ujumbe huo wa FIFA kwa msaada mkubwa katika historia ya mahusiano kati ya FIFA na TFF. Ujio huo unafuatia maombi ya TFF kuwa sehemu ya mradi wa Performance wa FIFA. Mradi wa Performance unaoshirikisha nchi mashirikisho 163 kati ya wanachama 209 wa FIFA, unalenga kuongeza ufanisi katika uendeshaji na uongozi wa nchi wanachama wa FIFA.