RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amezitaka halmashauri nchini kuepukana na vishawishi vya kutumia fedha za maendeleo ya wananchi kulipia posho za vikao vya madiwani. Rais Kikwete ametoa maelekezo hayo Oktoba 10, 2014, wakati alipozungumza na wananchi na viongozi wa Mkoa wa Mwanza wakati anaweka jiwe la msingi la ujenzi wa Barabara ya Usagara-Kisesa kwa kiwango cha lami katika sherehe ya kufana iliyofanyika Kisesa, kilomita 16 kutoka mjini Mwanza.
Rais amelazimika kutoa maelekezo hayo baada ya kujulishwa na Waziri wa Ujenzi, John Pombe Magufuli kuwa kwa mwaka huu wa fedha, Mkoa wa Mwanza utapewa kiasi cha Sh. bilioni 7.2 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa barabara za Mkoa huo ambao ziko chini ya Halmashauri za Mkoa huo nyingi zikiwa za vijijini.
Fedha hizo kutoka Mfuko wa Barabara ni kiwango kikubwa zaidi cha fedha ambazo zimepata kutolewa kwa Mkoa huo kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa barabara za halmashauri ambazo haziko chini ya Wakala wa Barabara wa Tanroads.
“Fedha hizi ni nyingi. Kwa kweli kwa sasa, tatizo siyo upatikanaji wa fedha. Tatizo ni mchwa unaotafuna fedha hizi za umma. Kwa hiyo fedha hizo nyingi ambazo mnapewa msizitumie kulipia posho za madiwani. Jipangeni vizuri, zitumieni vizuri fedha hizo,” amesema Rais Kikwete.
Rais Kikwete ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara hiyo ya Usagara-Kisesa yenye urefu wa kilomita 16.95 ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku tatu ya kikazi katika Mkoa wa Mwanza. Rais Kikwete aliwasili Mwanza, Oktoba 9, 2014 akitokea Kampala, Uganda ambako alikuwa Mgeni Maalum katika Sherehe za Miaka 52 ya Uhuru wa Uganda zilizofanyika kwenye Viwanja vya Sherehe vya Kololo mjini humo.
Barabara ya Usagara-Kisesa ambayo ni pamoja na ujenzi wa daraja kubwa la Nyanshishi inagharimu kiasi cha Sh.17.895 bilioni mbali na kiasi cha Sh. milioni 122 ambacho kimetolewa na Serikali kufidia wananchi ambao mali zao zitaharibiwa kupisha ujenzi wa barabara hiyo.
Barabara hiyo inalenga kurahisisha usafiri kati ya Mikoa ya Mwanza, Simiyu, Mara na Kagera ambako sasa wasafiri hawatakuwa tena na ulazima wa kuingia katikati ya Jiji la Mwanza ili kuendelea na safari zao.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa Tanroads, Injinia C. Ako amemwambia Rais Kikwete kuwa ujenzi wa barabara hiyo unafanywa na kampuni ya kizalendo ya Nyanza Road Works Limited na imepangwa kumalizika katika kipindi cha miezi 15.
Baadaye, Rais Kikwete amefungua Daraja la Wavukaji Barabara kwa miguu katika eneo la Mabatini mjini Mwanza ambalo limepunguza kwa kiasi kikubwa madhara ya watu kugongwa na magari na pia limepunguza msongamano wa magari katika eneo hilo la barabara ya Mwanza – Musoma.
Barabara hiyo inapitisha magari 30,000 kila siku na takwimu zinaonyesha kuwa wastani wa watu wanane walikuwa wanagongwa na magari katika eneo hilo la Mabatini na kati ya hao wawili walikuwa wanapoteza maisha. Rais Kikwete, amezindua Jengo la Kitega Uchumi la Shirika la PPF lililoko katikati ya Jiji la Mwanza, ikiwa ni sehemu ya ziara yake katika Mkoa wa Mwanza.