• Ni mkali wa lugha tano ikiwamo Kiswahili
• ‘Alishuhudia’ MV Bukoba ikizama
Joseph Hiza na Mashirika ya Habari
KIONGOZI wa Mtandao wa Kigaidi wa Al-Qaeda kwa ukanda wa Afrika Mashariki, Fazul Abdullah Mohammed ameuawa na Jeshi la Serikali ya Mpito la Somalia usiku wa kuamkia Jumatano ya wiki iliyopita.
Kifo hicho ni pigo kubwa katika utekelezaji wa operesheni za mtandao huo eneo hili na kwingineko kwa ujumla wake.
Kuuawa kwake kunaliingiza kundi hilo katika majonzi makubwa ikiwa ni mwezi mmoja tu tangu kuuawa kwa kiongozi mkuu wa mtandao huo duniani, Osama
Lakini dhima na kazi yake aliyoijenga katika miaka mchache iliyopita kama mkufunzi wa wanamgambo wapya huenda ikawa imeacha tishio kubwa kwa usalama wa eneo hili sasa na siku za usoni.
Kwa mujibu wa polisi wa Somalia, Fazul Mohamed, aliyekuwa akisakwa kwa muda mrefu na aliyekuwa mtaalamu wa kupanga mashambulizi, kujificha, kukwepa kukamatwa na mahiri katika kuzungumza lugha mbalimbali aliuawa wakati wa mrushiano wa risasi katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.
Maafisa wa Somalia juzi walisema Fazul ambaye Marekani ilimtangazia ‘bingo’ yenye thamani ya dola za Marekani milioni tano kwa yeyote atakayetoa taarifa zitakazosaidia kukamatwa kwake, aliuawa akiwa na mtuhumiwa mwingine wa ugaidi baada ya kufyatuliana risasi na polisi kwenye kizuizi cha barabara karibu na Mogadishu.
Kufuatia kifo cha Fazul Mohammed, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hillary Clinton, alikaribisha habari hiyo akiwa ziarani nchini Tanzania.
Aliwaambia waandishi wa habari kuwa kifo cha Fazul Abdullah Mohamed ni ‘pigo kubwa’ kwa al-Qaeda na washirika wake katika kanda hiyo.
Tangazo la vifo hivyo lilicheleweshwa kusubiri vipimo vya DNA kuthibitisha utambulisho wake pamoja na picha.
Awali askari waliomuua hawakuwa wamemtambua.
“Tulimzika,” anasema Jenerali Abdikarim Yusuf Dhagabadan, Naibu Mkuu wa Jeshi la Somalia.
“Lakini mara tulipokagua nyaraka zake, na kubaini kitu tuliufukua mwili wake na kuchukua picha na vipimo vya DNA.
Tukabaini ni mtu aliyekuwa akisakwa na mamlaka za Marekani.”
Jenerali huyo anakieleza kifo hicho kama kile cha Osama bin Laden.
“Ni ushindi kwa dunia. Ni ushindi kwa Jeshi la Somalia,” anaongeza.
Mkuu huyo wa Al-Qaeda Afrika Mashariki alikuwa katika gari aina ya Pickup lililokuwa limejaa dawa, kompyuta za laptop na simu za mkononi akijaribu kuelekea katika eneo linalodhibitiwa na waasi.
Inaonekana Fazul na mwenzake ambaye baadaye alikuja fahamika kuwa Ali Dele walifanya kosa lililowagharimu katika kizuizi cha barabara na walikataa kusimama, kwa mujibu wa maofisa, hali iliyosababisha kufyatuliana risasi kulikogharimu maisha yao.
“Vikosi vyetu viliwafyatulia risasi wawili hao waliokataa kusimama katika kizuizi cha barabara. Walijaribu kujitetea walipozingirwa na askari wetu,” Abdikarim analiambia Shirika la Habari la Ufaransa (AFP).
“Tulichukua vitambulisho vyao ikiwamo hati za kusafiria za kigeni pamoja na dawa, simu za mkononi na kompyuta za laptop,” anaongeza.
Maofisa wa Somalia wamesema Fazul alikuwa amebeba kiasi cha dola za Marekani 40,000 taslimu na hati ya kusafiria ya Afrika Kusini ikiwa na jina ‘Daniel Robinson.’
Pasi hiyo iliyotolewa Aprili 13, mwaka juzi, ikionyesha aliondoka Afrika Kusini Machi 19, 2011 kuelekea Tanzania, ambako alipewa kibali cha kuingia.
Fazul Mohammed anayejulikana kwa jina lingine la Harun, ni mshukiwa mkuu wa mashambulizi ya mwaka 1998 katika balozi za Marekani mjini Dar es Salaam-Tanzania na Nairobi-Kenya, yaliyoua watu 240.
Inaaminika mzaliwa huyo wa Comoro pia alipanga shambulio la mwaka 2002 dhidi ya hoteli inayomilikiwa na Wayahudi mjini Mombasa, Kenya na kusababisha vifo vya watu 15.
Lakini katika miaka michache iliyopita, baadhi ya wasomi na wataalamu wa masuala ya usalama waliamini Fazul Mohamed alikuwa akitumia muda mwingi kutoa mafunzo kwa wanamgambo na kuanda mipango ya kushambulia nchi za magharibi.
Alikuwa akitoa mafunzo kwa vijana wa Kisomali na Waislamu wengine waliokwenda Somalia kupata ujuzi na utaalamu wa kijeshi.
Profesa Nelly Lahoud, wa Kituo cha Kukabiliana na Ugaidi katika Chuo cha Kijeshi cha West Point nchini Marekani anasema, Fazul Mohammed alikuwa mtu muhimu katika kupanga operesheni za mtandao wa al-Qaeda.
Amesema kifo chake ni hasara kubwa kwa mtandao huo ingawa jukumu lake la kama mkufunzi bila shaka limelinufaisha kundi hilo.
Profesa Lahoud aliyepitia kitabu kilichoitwa ‘Vita dhidi ya Uislamu: Hadithi ya Fazul Harun’ ambacho huelezea maisha ya Fazul Mohammed, amesema mwanamgambo huyo ametoa mchango mkubwa kwa mtandao huo.
Kwa maoni yake, Fazul Mohamed alihisi kuwa aliwajibika kuwapa wenzake ujuzi aliokuwa nao.
Serikali ya Somalia imesema mamia ya wapiganaji wa kigeni walijiunga na mtandao huo, wakitokea nchi mbalimbali ikiwamo Afghanstan, Pakistan, nchi za Ghuba na Magharibi zikiwamo Marekani na Uingereza.
Baadhi yao wamekuwa viongozi wa makundi ya wanamgambo kama vile al Shabaab.
Maafisa wa usalama wa Magharibi pia walikuwa wakishuku kuwa Fazul Mohammed alikuwa akiratibu harakati zao pamoja na wanamgambo wa tawi la al Qaeda nchini Yemen.
Hilo ni tawi lililohusika na mashambulizi makali yaliyoendeshwa nalo katika nchi za magharibi, miaka ya hivi karibuni.
Waliomchunguza Fazul wanasema alikuwa mtu makinifu na mjanja na aliyezungumza kwa ufasaha lugha za Kiarabu, Kifaransa, Comoro, Kiswahili na Kiingereza.
Muaustralia Leah Farrellm mtaalamu wa masuala ya al-Qaeda, amesema kifo cha Fazul Mohamed kitaathiri uwezo wa al-Qaeda kuwepo katika kanda hiyo pamoja na operesheni zake katika nchi za kigeni.
Baadhi wa wataalamu wa masuala ya usalama, wanashuku kwamba mafunzo yaliyotolewa na Fazul Mohammed yamesaidia kupanga shambulio lililofanywa na kundi la al-Shabab mjini Kampala, Uganda mwaka 2010.
Shambulio hili lilisababisha vifo vya watu 79 waliokuwa wakiangalia kupitia runinga fainali ya Kombe la Dunia.
Hilo lilikuwa shambulio la kwanza kabisa kufanywa na al Shabab katika ardhi ya kigeni, kwa kile ilichosema kulipiza kisasi kwa Uganda kuchangia askari katika kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (AMISOM).
Katika shambulio lingine, wanamgambo wa al-Shabaab walishambila kambi kuu ya jeshi la Umoja wa Afrika (AU) Septemba 2009, mjini Mogadishu na kusababisha vifo vya askari 17.
Wakati meli ya MV Bukoba ilipozama katika Ziwa Victoria mwaka 1996, ikiwa imembeba mwanzilishi mwenza wa al-Qaeda, Abu Ubaidah al-Banshiri, Fazul alikuwa mmoja wa watu waliotumwa eneo la tukio, kujaribu kuthibitisha iwapo Abu Ubaidah ni miongoni mwa waliokufa, kitu ambacho hawakukosea
Mbali ya shambulio la balozi za Marekani mjini Dar es Salaam na Nairobi, mwaka 2002, Fazul alishutumiwa kuhusika na mashambulizi dhidi ya Hoteli ya Kikambala mjini Mombasa, Kenya na jaribio la kuidungua ndege ya Israel mjini humo.
Mapema mwaka 2007 wakati wa vita ya Somalia, Fazul alidhaniwa kuwa mpakani katika Kijiji cha Haya karibu na Ras Kamboni, sambamba na wanamgambo wa uliokuwa Umoja wa Mahakama za Kiislamu (ICU).
Januari 8, 2007, ndege ya Jeshi la Anga la Marekani, AC-130 ilishambulia eneo hilo, katika kile kilichoonekana kumlenga.
Maofisa wa Somalia walidai kifo chake kimethibitishwa kwa mujibu wa taarifa za Marekani kwa Serikali ya Somalia, lakini Balozi wa Marekani nchini Kenya, Michael Ranneberger, alikana kuuawa kwa Fazul katika shambulio hilo akisema kwamba msako dhidi yake na wenzake bado unaendelea
Mmoja wa wake zake na watoto wake walikamatwa wakijaribu kukimbilia Kenya kutokea Somalia.
Lakini Serikali ya Kenya ikawarudisha Somalia, ikikamata kompyuta ya mumewe iliyokuwa na taarifa nyeti.
Fazul anaaminika kuwa mtaalamu mkubwa wa kompyuta.
Kwa mara ya kwanza Fazul aliingia katika anga za wapelelezi wa Marekani baada ya mashambulizi dhidi ya balozi zake Kenya na Tanzania.
Ameelezwa na Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI) kama mtaalamu wa kutumia majina bandia aliyewakwepa kwa miaka mingi.
Anasemekana alielekea nyumbani katika visiwa vya Comoro vilivyopo Bahari ya Hindi mara baada ya shambulio hilo, lakini wakati makachero wa FBI walipombaini, alipanda ndege kuelekea nchi za Ghuba na kutoweka machoni mwao.
Fazul Abdullah aliyezaliwa visiwa humo katika miaka ya 1970, inaaminika alijiunga na al-Qaeda nchini Afghanistan katika miaka ya 1990.
Anasemekana alitumikia kipindi fulani akisoma nchini Saudi Arabia.
Kikosi cha Kupambana na Ugaidi cha Marekani kilipata hati ya kusafiria ya Fazul Abdullah Mohammed iliyotolewa mwaka 1990 mjini Moroni na kufufuliwa mwaka 1996 mjini Jeddah, Saudi Arabia.
Hati hiyo ilionesha alisafiri kwenda Mauritius mwaka 1990, Tanzania mwaka 1994 na Sudan mara kadhaa mwaka 1995 ambapo pia alikuwa Yemen na Kenya mwaka 1993 na mara kadhaa 1994 na 1995.
Inaonesha pia alikaa kwa mwaka mmoja nchini Pakistan 1991-1992.
Hakuwa akijulikana sana kabla ya hapo na tukio la mashambulizi ya mwaka 1998 nchini Tanzania na Kenya ndilo lililomuibua.
Alikuwa akishikilia uraia wa Comoro na Kenya ambako alioa na aliishi akifanya kazi kama mwalimu wa dini ya Kiislamu.
chanzo: gazeti la Mtanzania