NA HASSAN SILAYO
SERIKALI imewataka watendaji serikalini kuzifanyia kazi tafiti mbalimbali zinazotolewa na asasi za kiraia ili kuleta matokeo chanya na kuboresha maisha ya watanzania. Hayo yamesemwa leo na Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI Seleman Jafo wakati akipokea ripoti ya Takwimu Mpya za Uwezo Tanzania iliyopo katika TWAWEZA.
Akiongea katika Hafla hiyo Naibu Waziri Jafo amesema kuwa Watendaji Serikalini sasa wana budi wa kufanyia kazi tafiti mbalimbali zinazotolewa na Azaki za kiraia zinazolenga masuala yaliyopo katika jamii ili kuiwezesha serikali kuyafanyia kazi matokeo ya tafiti na kuboresha hali ya watanzania.
“Kwa matokeo haya ya Tafiti ya TWAWEZA kupitia Uwezo Tanzania ni kipimo tosha cha kutuonesha sisi kama viongozi yapi tunayotakiwa kufanya na yapi hatutakiwi kufanya na yapi tunatakiwa tuyarekekebishe katika sekta ya elimu na matokeo haya tutayafanyia kazi”-Naibu Waziri Jafo.
Aidha Naibu Waziri Jafo aliwastaka wabunge kutumia vikao muhimu vya kisheria kwenye maeneo yao ya kazi katika kuhakikisha matokeo ya tafiti yanasaidia kuboresha sekta ya elimu katika Halmashauri huku serikali ikiendelea kuwekeza katika sekta ya elimu.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza Aidan Eyakuze alisema kuwa tathmini hii inayopima matokeo ya kujifunza ambayo ambayo ni kubwa barani afrika inayotekelezwa kwenye baadhi ya nchi ikiwamo Kameruni, Nigeria, Senegali,Mali, Ghana na Burkina Faso inasaidia kuonesha hali halisi ya iliyopo mashuleni ili kuboresha sekta ya elimu.
Naye Meneja wa Uwezo Tanzania Zaida Mgalla amewataka viongozi wa Serikali na wabunge kutumia tafiti hii ya uwezo katika kuhakikisha wanashiriki katika kuboresha elimu katika maeneo yao na Tanzania kwa Ujumla ikiwa ni lengo kuu la kuhahakikisha wanaifikisha sekta ya elimu pale inapotakiwa.