Familia Newala Zachangia Kuwalinda Wanyanyasaji

Mkuu wa Polisi Wilaya ya Newala (OCD), Jeremiah Shila akionesha vitabu ambavyo hutumika kutoa mafunzo kazini kuwanoa askari hasa wa Dawati Maalum la Jinsia na Watoto.

Mkuu wa Polisi Wilaya ya Newala (OCD), Jeremiah Shila akionesha vitabu ambavyo hutumika kutoa mafunzo kazini kuwanoa askari hasa wa Dawati Maalum la Jinsia na Watoto.

Mjumbe wa Dawati la Jinsia la Jeshi la Polisi Wilaya ya Newala, Yusta Timoth (askari) akizungumza na mwandishi wa habari hizi kuelezea jitiada za dawati hilo katika kukabiliana na vitendo vya kikatili kwa jamii.

Mjumbe wa Dawati la Jinsia la Jeshi la Polisi Wilaya ya Newala, Yusta Timoth (askari) akizungumza na mwandishi wa habari hizi kuelezea jitiada za dawati hilo katika kukabiliana na vitendo vya kikatili kwa jamii.

MKUU wa Polisi Wilaya ya Newala (OCD), Jeremiah Shila amesema baadhi ya wanafamilia wilayani hapo wamekuwa kikwazo kwa mapambano dhidi ya vitendo anuai vya kikatili kwa kile kuwalinda watu wanaokabiliwa na kesi hizo. OCD Shila alitoa kauli hiyo hivi karibuni alipokuwa akizungumzia utendaji wa Dawati Maalum la Jinsia na Watoto la Wilaya hiyo dhidi ya vitendo vya unyanyasaji.

Mkuu huyo wa Polisi Wilaya ya Newala, mbali na kukiri Dawati Maalum la Jinsia na Watoto kupokea kesi kadhaa za unyanyasaji wa kijinsia alisema baadhi ya wanafamilia na wananchi wengine wanaopaswa kutoa ushirikiano wamekuwa na tabia ya kulindana kifamilia kwa kuoneana aibu na pengine kumalizana nje ya vyombo vya sheria jambo ambalo ni changamoto katika kukabiliana na vitendo hivyo.

“…Watu wanafanyiwa vitendo kama hivi kisha wao wanamalizana wenyewe nje ya vyombo vya sheria…unakuta wanalipana, unakuta mtoto wa shule kaachishwa shule kwa mimba au kutoroshwa wahusika wanalindana na kuyaficha kisha wanayamaliza nje ya utaratibu wa kisheria,” anasema.

“…Upo pia mchezo wa wahusika kujificha mara baada ya kosa nap engine husafiri na kwenda kujificha nje ya mkoa kwa miaka miwili hadi mitatu na kurejea baadaye jambo ambalo linakuta kesi imefutwa,” alisema OCD, Shila akizungumza na mwandishi wa habari hizi.

Alitolea mfano kesi za mimba kwa wanafunzi zimekuwa zikichelewa kutolewa taarifa mara baada ya kosa na wanapozifuatilia hubaini kosa lina zaidi ya miezi mitatu na wahusika hukuta tayari wamekimbia eneo hilo jambo ambalo huwa changamoto kwa Polisi.

Hata hivyo alisema ili kukabiliana na kesi hizo elimu hainabudi kutolewa kwa nguvu kuanzia shuleni kwenyewe na jamii kwa ujumla kuifanya iwe tayari kuvipinga kwa dhati vitendo hivyo. Alisema mkono wa sheria nao unatakiwa kutumiwa kwa kiasi kikubwa ili kuwafanya jamii ielewe dhana ya kutii sheria bila shuruti.

Kwa upande wake, Mjumbe wa Dawati la Jinsia la Jeshi la Polisi Wilaya ya Newala, Yusta Timoth alisema kuna ukatili wa kijinsia katika kundi la wanawake, watoto na hata wanaume, matukio ambayo hujitokeza pia katika taarifa za kesi zao na kuyafanyia kazi inavyowezekana.

Akitoa takwimu za matukio ya kesi zilizolifikia dawati hilo tangu mwezi Januari –Septemba 2014 katika kituo hicho; anasema jumla ya kesi za GBV 101 ziliwafikia, huku ubakaji 19 ziliripotiwa, kulawiti zilikuwa kesi 5, kujeruhi kesi 20 (vipigo), shambulio kesi 32, kudhalilisha kwa matusi kesi 24, mimba kwa wanafunzi kesi 3.
*Imeandaliwa na www.thehabari.com