Fainali Copa Cocacola zazikutanisha Morogoro na Mwanza


FAINALI ya michuano ya Copa Coca-Cola 2012 inayozikutanisha timu za Mwanza na Morogoro itachezwa kesho (Julai 15 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam kuanza saa 9 kamili alasiri.

Mwanza ilipata tiketi ya kucheza fainali baada ya kuifunga Temeke mabao 3-1 wakati Morogoro iliiondoa Tanga kwenye nusu fainali kwa ushindi wa mabao 3-1. Mechi zote za nusu fainali zilichezwa Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume.

Mechi ya kutafuta mshindi wa tatu kati ya Temeke na Tanga itachezwa kwenye uwanja huo huo kuanzia saa 5 asubuhi. Mashindano ya Copa Coca-Cola 2012 yalianza Juni 24 mwaka huu yakishirikisha mikoa 28 ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Na wakati huo huo Kozi ya makocha wa mpango wa grassroots unaolenga wachezaji mpira wa miguu (wasichana na wavulana) wenye umri kuanzia miaka 6-12 inafungwa kesho (Julai 15 mwaka huu) saa 4.30 asubuhi kwenye ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Makocha hao walianza kunolewa Julai 10 mwaka huu kwenye ukumbi wa Msimbazi Center, Dar es Salaam na wakufunzi kutoka Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) wakiongozwa na Gouinden Thandoo.

Washiriki wa kozi hiyo walikuwa 35 ambao ni makocha wa timu mbalimbali zilizoshiriki mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma wa Shule za Msingi Tanzania (UMITASHUMTA).