Na Mwandishi Wetu
BODI ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), imeagiza Mtendaji Mkuu na Mwenyekiti wa Kampuni ya BP Tanzania Ltd wafikishwe mahakamani mara moja.
EWURA imetoa agizo hilo kupitia kwa Mkurugenzi wa Mashitaka ya Jinai (DPP), na imetaka washtakiwe kwa kukiuka Sheria ya mamlaka hiyo.
EWURA pia imesitisha leseni ya biashara ya kampuni hiyo ya BP kwa muda wa miezi mitatu kuanzia leo Agosti 12 mwaka huu, hivyo hawataruhusiwa kuuza mafuta ya taa, petroli na wala dizeli.
Kauli hiyo imetolewa leo na Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Haruna Masebu jijini Dar es Salaam alipokuwa akitangaza hatua ambazo mamlaka hiyo imechukua dhidi ya kampuni za mafuta zilizokuwa na mgoma baridi tangu Agosti 3, 2011.
Masebu alisema kampuni ya BP (T) Ltd itaruhusiwa kuendelea kuuza mafuta ya ndege kwa kuwa EWURA haidhibiti bei za mafuta hayo ambao ndiyo msingi wa mgomo kwa wafanyabiashara wa mafuta.
“BP hataruhusiwa kuuza mafuta ya petroli, dizeli na ya taa yaliyopo kwenye maghala yake kwa wafanyabiashara wengine wa jumla kama wanataka, lakini chini ya usimamizi wa EWURA tu.
“…Tumewaruhusu kufanya hivi ili kuzuia kutoharibika kwa mafuta hayo katika kipindi hicho cha miezi mitatu, ambapo hataruhusiwa kufanya biashara ya mafuta ya jumla,” alisema Masebu.
Aliongeza vituo vyote vya rejereja (petrol stations) vyenye nembo ya BP vitaruhusiwa kuuza mafuta kwa kununua mafuta kwa wafanyabiashara wengine wa jumla na si kwa BP.
Katika hatua nyingine EWURA imeziandikia onyo kali kampuni za Oilcom (T) Ltd, Camel Oil (T) Ltd, na Engen Petroleum (T) Ltd na kuzionya kutorudia tabia walioyoionesha, ambayo ni kinyume na sheria za Tanzania.
Pia imeziagiza kampuni hizo ziuze mafuta kwa watu wote bila ubaguzi na kueleza kuwa amri hiyo itafuatiliwa kwa karibu na ikibainika wamekiuka hatua kali zaidi zitachukuliwa dhidi yao.
Masebu alisema kuanzia sasa, EWURA itaendelea kuangalia mfumo mzima wa mafuta yanayoingia bandarini, pamoja na kufuatilia bei zinazouzwa kwenye vituo kama zinafanana na zile zilizotangazwa.