Na Belinda Kweka – Maelezo
MAASKOFU na Wachungaji wa kanisa la ‘Good News For All Ministry’ wametoa sababu zilizochangia Timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ kufungwa katika mechi yao na Timu ya Ivory Coast iliyofanyika Juni 16, mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari leo katika ukumbi wa mikutano wa Idara ya Habari – MAELEZO jijini Dar es Salaam, Askofu Charles Gadi amesema kuwa kuna sababu nyingi zilizosababisha Taifa Stars kushindwa katika mchezo wake na Ivory Coast ikiwa ni pamoja na matusi na mzaha unaofanywa na wananchi wenyewe uwanjani.
“Ndugu waandishi, ni kweli goli la kwanza lilifungwa kwa maombi ya Watanzania waliokuwa wakiomba, lakini matusi yaliyoendelea pale uwanjani ambayo yanatukana maumbile ya mama, dada, wakwe na watoto zetu wa kike yalitukwamisha.
“Unapotukana kwa kutumia maumbile ya wakina mama ni sawa na kuchafua,kujeli uumbaji wa Mungu kwa wakina mama. Hali hiyo hutuletea laana ya kushindwa,” alisema Askofu Gadi.
Aliongeza kuwa walianza kuiombea Taifa Stars toka mwaka 2012 ili ifanikiwe katika mechi zake zote hivyo wana uchungu kwa kufungwa na timu hiyo ya kigeni.
Aidha Askofu Gadi aliongeza kuwa pale uwanjani kulikuwa kumefurika watu wengi hivyo kuhatarisha usalama wa watu walioko pale na hivyo ameiomba Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) litoe tiketi kulingana na idadi ya viti vilivyopo uwanjani.
Pia Askofu Gadi amesema kuwa wana maombi ya siku elfu moja kwa ajili ya kuliombea Taifa zima, mpaka sasa wamekaribia siku mia tano katika maombi hayo hivyo wanaomba watu kutokwamisha maombi yao kwa kuacha matusi.
“Naomba Watanzania wamwogope Mungu kwa kuacha matusi na dhambi zao kwani wakifanya hivyo nchi itakuwa na maendeleo na kuwa ya kistaarabu kwa kuendeleza amani,” alisisitiza Mchungaji Leonard Kijuna.
Pia Askofu Gadi ametoa wito kwa Serikali kuwa waweze kutunga sheria kuhusu matusi kwamba endapo mtu atapatikana akitukana basi achukuliwe hatua kama zilivyo nchi njingine,mtu akitupa bigijii anafungwa, kwani itasaidia kutokomeza kabisa suala hilo.