Endrew Laiser ajitosa Uenyekiti (UVCCM) Musoma

vijana wa CCM Taifa

MJUMBE wa Baraza la umoja wa vijana wa CCM Mjini Musoma (UVCCM) na mweka hazina wa Umoja huo Endrew Simon Laiser amejitosa kuwania nafasi ya Mwenyekiti wa Umoja huo katika Manispaa ya Musoma na kuahidi kuleta mabadiliko makubwa katika Umoja huo na kuwafanya Vijana kurudisha imani katika chama na kuendelea kukipenda,

Akizungumza na Waandishi wa Habari mara baada ya kuchukua fumu ya kuwania nafasi hiyo katika ofisi ya Umoja wa Vijana Wilaya,Endrew alisema kwa sasa Umoja huo umekuwa ukisusua kutokana na kutokuwa na mipango madhubuti ya kuwajenga Vijana ikiwa ni pamoja na kuwa miradi ambayo itawawezesha kujiingizia kipato huku wakiwa wanaendelea kufanya kazi za Siasa.

Alisema cha kwanza atakachoanza kukifanyia utekelezaji mara baada ya wajumbe wa mkutano mkuu wa uchaguzi watakapo muamini na kumchagua katika nafasi hiyo atahakikisha miradi yote iliyokuwepo ya umoja huo pamoja na miradi mipya inakuwa hai na kushirikiana na asasi mbalimbali za kijamii katika kuwajengea uwezo vijana katika kusimamia miradi hiyo.

Endrew alisema haiwezekani kwa siasa za sasa katika Nchi hii kuzifanya bila kuwa na Vijana mbao watakuwa na shughuli za kuwaingizia kipato na kutumiwa na wagombea katika nafasi mbalimbali kipindi cha uchaguzi na kudai kuwa mfumo kama huo ndio unaowafikisha vijana katika hali waliyo nayo kwa sasa.

“Vijana tumekuwa tukitumiwa kama ngazi ya kupandia katika kutafuta nafasi za viongozi katika chaguzi mbalimbali kisha tunaachwa hadi katika kipindi kingine cha uchaguzi,mimi ntahakikisha mfumo huo unabadilika kwa kuwafanya vijana kuwa na miradi yao na watafanya kazi ya siasa mara baada ya kuingiza kipato kutoka katika miradi yao,”alisema Endrew..

Alisema baadhi ya vijana wamekuwa wakijiondoa katika Umoja na ndani ya Chama na kujiunga na vyama vya Upinzani na hiii ni kutokana na kuto kuwekewa mipango mizuri ambayo itawafanya kujiingizia kipato na kuachwa kwa muda mrefu bila kuwashirikisha katika mambo yanayohusiana na mikakati ya Chama katika kuwajengea uwezo vijana.

Aidha mgombea huyo wa nafasi ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Musoma Mjini alisdema suala la uanzishaji wa Saccos ya vijana ni suala la muhimu litakalo wafanya kujiwekea akiba zao zinazotokana na michango yao katika Saccos na baadae kupata mikopo yenye riba nafuu ambayo itawafanya kujimudu kimaisha.

Alitoa wito kwa vijana kujiepusha na viongozi watakaotaka nafasi kwa misingi ya kutoa rushwa katika uchaguzi kwa kusema viongozi wa namna hiyo sio wawajibikaji na ndio waliowafikisha vijana na umoja wao hapo ulipo na kuelekea kupoteza imani kwa vijana.

“Mimi nawaomba vijana wenzangu watafakari kabla ya kuchagua viongozi ambao watawaletea mabadiliko,suala la rushwa na madai ya posho ambazo hazina tija ndio zimetufikisha tulipo kwa sasa na kama tunahitaji mabadiliko tujiepushe na masuala haya ya rushwa na posho na kufanya kazi za chama na umoja kwa moyo,”aliongeza Endrew.

Fomu za kuwania nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi w Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Mjini Musoma zimeanza kutolewa Mei 2 Mwaka huu huku mwisho wa kuchukua na kurudisha fomu hizo ikiwa ni Mei 10.