MJUMBE wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Eliud Mvella amejiondoa kwenye mchakato wa uchaguzi uliopangwa kufanyika Oktoba 27 mwaka huu.
Mvella amemwandikia barua Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Hamidu Mbwezeleni akielezea uamuzi wake huo pamoja na mambo mengine umetokana na kile alichodai kuwa Kamati hiyo haikumtendea haki kwa kumwondoa.
Mbwezeleni amekiri kupokea barua hiyo, na kuongeza kuwa licha ya uamuzi huo wa Mvella aliyekuwa ameomba kuwania ujumbe wa Kamati ya Utendaji kupitia Kanda Namba Saba ya mikoa ya Iringa na Mbeya, bado suala lake litasikilizwa na Kamati ya Maadili ya TFF kwa ajili ya hatua zaidi.
Kamati ya Mbwezeleni ilimuondoa Mvella katika kinyang’anyiro hicho kwa kushindwa kuheshimu Kanuni za Uwajibikaji wa Pamoja (collective responsibility) baada ya kushiriki kufanya uamuzi ndani ya Kamati ya Utendaji ya TFF bila ya kutaka msimamo wake wa kupinga uwekwe kwenye muhtasari na baadaye kuupinga uamuzi huo akiwa kwenye uongozi wa mkoa.
FDL SASA KUPIGWA UWANJA WA KAWAWA
Mechi za nyumbani za timu ya Kanembwa JKT ya Kigoma iliyoko Ligi Daraja la Kwanza (FDL) sasa zitachezwa katika Uwanja wa Kawawa badala ya ule wa Lake Tanganyika.
Uamuzi wa kuhamishia mechi hizo Uwanja wa Kawawa ulioko Ujiji umetokana na Uwanja wa Lake Tanganyika kutumiwa na Serikali katika Operesheni Ondoa Wahamiaji Haramu inayoendelea nchini kwa sasa. Uwanja huo hivi sasa unatumika kuhifadhi wahamiaji hao. Kanembwa JKT inaanzia nyumbani kwa kuikaribisha Polisi Tabora. Mechi hiyo itachezwa Jumamosi (Septemba 14 mwaka huu).
*Imeandaliwa na Boniface Wambura Mgoyo, Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)