RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa miongoni mwa malengo ya Mapinduzi ya Januari 12, 1964 ni kuhakikisha elimu inayotolewa Zanzibar inayafaa makundi yote yaani wenye uwezo na wasio na uwezo. Dk. Shein aliyasema hayo huko katika viwanja vya skuli ya Madungu mara baada ya kuifungua skuli mpya ya Sekondari ya Madungu iliopo Wilaya ya Chake, Mkoa wa Kusini Pemba ikiwa ni miongoni mwa shamrashamra za kutimia miaka 49 ya Mapinduzi matukufu ya Januari 12, 1964.
Alisema kuwa kabla ya Mapinduzi elimu ilikuwa ikitolewa kwa ubaguzi na matabaka maalum hali ambayo iliwanyima fursa wananchi waliowengi ambao walikuwa ni wanyonge na kueleza kuwa hata skuli zenyewe kwa wakati huo hazikuwepo za kutosha. Kutokana na hali hiyo mara tu baada ya Mapinduzi Rais wa Awamu ya Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar alitangaza elimu bila Malipo hatua ambayo iliwapelekea wenye uwezo na wasio na uwezo kupata fursa ya elimu.
Alieleza kuwa jambo kubwa hivi sasa linalopewa kipaumbele na serikali ni kuifanya elimu iwe bora zaidi hapa Zanzibar kwani tayari juhudi za kujenga majengo ya skuli Unguja na Pemba zimeshafanyika na mkazo utakuwa ni kuimarisha elimu ya msingi.
Dk. Shein aliwataka wazee na waalimu kuhakikisha wanatoa msaada mkubwa kwa vijana ili waweze kufanya vizuri katika masomo yao kwani wao wana nafasi kubwa katika maendeleo ya vijana hao. Alisisitiza kuwa Mapinduzi ni maendeleo, hivyo kujengwa kwa skuli hizo Unguja na Pemba kutakuwa ni kichocheo kikubwa cha maendeleo.
Alisema kuwa ahadi alioitoa katika Kampeni za uchaguzi uliopita ndio hiyo aliyoitimiza huku akisisisitiza kuwa licha ya serikali kuwa imekopa fedha za ujenzi wa skuli hizo lakini imetengeza skuli nzuri na zilizobora huku akiahidi kuwa ipo siku Serikali itazilipa fedha hizo ilizokopa kutoka Benki ya dunia.
Akitoa historia katika elimu Dk. Shein alisema kuwa ni lazima wananchi wajue elimu Zanzibar katika miaka ya nyuma ilikuwa ikitolewa kwa ubaguzi mkubwa hadi kufikia Mapinduzi ndipo wanyonge walio wengi nao walipata fursa hiyo.
Alisema kuwa hadi Mapinduzi wanafunzi wa Serkondari walikuwa 734 tu hapa Zanzibar na kwa upande wa Pemba kulikuwa na Skuli moja tu ya Sekondari ambapo leo zipo skuli za sekondari 62. Kidato cha kwanza hadi cha nne na za Msingi na Kati ziko 26 ambazo zote zinafanya idadi ya Skuli za Sekondari 88.
“Wareno wametawala karibu miaka 200 lakini hawakujenga skuli hata mmoja, na mfalme kajenga skuli moja tu ambaye alitawala zaidi ya miaka 140 je tuangalie Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ndani ya miaka 49 imejenga skuli ngapi,” alisema Dk. Shein.
Alisema kuwa kwa upande wa Wilaya hiyo ya Cheke hivi sasa skuli za A level zitakuwa nne katika na kufanya idadi ya skuli hizo kuwa 12 huku akieleza azma ya kuwepo Tawi la SUZA litakalofunguliwa huko Mchangamdogo Pemba.
Alieleza kuwa wanaotaka maendeleo ni lazima wasome, na kusema kuwa kuna haja ya kila mmoja asome hasa ikizingatiwa mabadiliko ya sanyansi na teknolojia yanayokuwa siku hadi siku sanjari na kuitumi Kompyuta kwa kazi mbali mbali za msingi. Alisema kuwa ni mradi wa mwanzo mkubwa katika sekta ya elimu kwa Zanzibar. Dk. Shein alitoa shukurani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutoa ushirikiano mkubwa katika kuhakikisha fedha zilizojenga skuli hizo 21 hapa Zanzibar zinapatikana na inakabidhiwa Zanzibar katika kutekeleza mradi huo.
Naye Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Ali Juma Shamuhuna alimshukuru Rais Jakaya Mrisho Kikwete kwa kusimama kidete katika kuhakikisha Zanzibar inakopeshwa fedha za kuendeshea mradi huo kutoka Benki ya Dunia. Pia, alitoa pongezi kwa Rais Mstafu wa awamu ya sita Mhe. Amani Abeid Karume kwa kuhakikisha kuwa Zanzibar inakopeshwa fedha hizo ambazo zimeweza kutumika vizuri na kila mmoja anaona matunda yake.
Mapema Naibu Katibu wa Wizara hiyo, Maalim Abdala Mzee alisema kuwa mradi huo ulianza Juni 2007 na unatarajiwa kumaliza Juni mwaka huu huku akisisitiza kuwa kukamilika kwa skuli hizo kutaongeza idadi ya Skuli za Sekondari kufikia nne katika Wilaya hiyo ya Chake. Alieleza kuwa zaidi ya Shilingi Bilioni 62.7 zinatarajiwa kutumika katika mradi huo ambapo utakuwa na skuli 19 za Sekondari,pamoja na chuo cha waalimu huko Pemba na skuli 6 za sekondari zinazofanyiwa matengenezo pamoja na vifaa, vitabu, thamani na mafunzo ya waalimu.