Elias Kerenge kugombea uenyekiti UVCCM-MARA

Baadhi ya wanachama wa UVCCM wakiwa katika shughuli za kichama

Na Shomari Binda wa Binda News-Musoma

MJUMBE wa Baraza la umoja wa vijana wa CCM (UVCCM) Mkoa wa Mara na Mwenyekiti wa umoja huo kata ya Mwigobero katika Manispaa ya Musoma Elias Selemani Kerenge ametangaza nia ya kuwaania nafasi ya Mwenyekiti wa Umoja huo Mkoa wa Mara na kuahidi kuleta mabadiliko makubwa katika umoja moja ikiwa ni pamoja na kuanzisha Saccos kubwa kwa ajili ya maendeleo ya Vijana.

Elias ametangaza nia hiyo hii leo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Hotel ya Afrux na kusema umefika wakati wa vijana kuomba nafasi huku wakiweka malengo ya kuhakikisha vijana wenzao wanakuwa na mabadiliko ya kimaisha kupitia miradi mbalimbali ya kimaendeleo na si muda wote kukaa na kuzungumzia habari za kisiasa.

Amesema kuwa iwapo muda ukifika na mkutano mkuu wa uchaguzi wa umoja huo ukamuamini na kumpa nafasi hiyo atahakikisha anaitumia vizuri miradi ya umoja huo kama kitega uchumi cha Vijana wote wa Mkoa wa Mara kwa kushauriana na viongozi wengine ili kuona ni namna gani miradi hiyo inaweza kuwanufaisha vijana na kupata maendeleo.

“Umoja wetu wa Vijana unayo miradi mingi ikiwemo jengo kubwa la kitega uchumi lililopo katika Manispaa ya Musoma pamoja na miradi mingine ambayo ipo karibu Wilaya zote na hii ikipata usimamizi mzuri itawanufaisha vijana kiuchumi huku wakiendelea kufanya shughuli zinazohusu (UVCCM) pamoja na zile za Chama chetu cha Mapinduzi,” alisema Elias.

Amedai ili kupata usimamizi mzuri wa miradi hiyo na kuiendeleza kutaandaliwa mafunzo mbalimbali ya ujasiliamali kutoka kwa wataalamu wa shghuli za ujasiliamali na kuwa karibu na maofisa na wataalamu wa Maendeleo ya jamii ili miradi itakayokuwepo iweze kuwanufaisha Vijana na kujikwamua katika maisha.

Amesema kuwa upande wa Upinzani umekuwa ukipata nafasi ya kuwapata vijana kutokana na kuwaeleza kuwa CCM haiwezi kuwaletea mabadiliko ya kimaisha lakini yeye amedai iwapo atapata nafasi ya kuwa Mwenyekiti wa umoja wa vijna wa CCM (UVCCM) Mkoa wa Mara ataelekeza nguvu zake katika shughuli za miradi na kuhakikisha inafunguliwa Saccos kubwa ya Umoja huo itakayowanufaisha vijana wote naa kuziba mianya ya kurubuniwa na Upinzani.

Ameeleza kuwa kupitia miradi hiyo kila Kijana atakuwa na nafasi kujishughulisha na kujipatia kipato na hakutakuwa na nafasi tena ya kijana kukimbilia katika vyama vya Upinzani kutokana na kurubuniwa kwa namna yeyote na vyama hivyo na lazima kuwepo na timu ya uhamasishaji vijana kuingia katika umoja wa Vijana .

“Nakumbuka mimi niliingia katika Chama cha Mapinduzi miaka 20 iliyopita na nilianzia Chipukizi nikiwa Shule ya msingi, ntahakikishia kunakuwepo na progaram maalumu ya kutembelea mashuleni na kuanzisha Chipukizi imara ili kurudisha hadhi ya Umoja wa Vijana kama ilivyokuwa zamani pamoja na kuanzisha makambi ya kupeana mafunzo ya maadili,” aliongeza.

Katika kuelekea katika uchaguzi wa (UVCCM)-Mkoa,Elias amewaomba Wanachama wa umoja huo kuwachagua viongozi makini katika uchaguzi wa Wilaya na kuacha kuwachagua viongozi wanaotumia Rushwa kwa kuwa viongozi wa namna hiyo ndio waliokifikisha Chama cha Mapinduzi katika mazingira ya kulaumiwa.

Amesema viongozi wanaopaswa kuchaguliwa ni wale wanaojituma na shupavu na wanaoweza kusimamia vizuri majukumu yao na kufanya utekelezaji wa mara moja kwa kile kinachohitaji utekelezaji kutoka kwa kiongozi.

Mtangaza Nia huyo wa nafasi ya Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM Mkoa wa Mara (UVCCM) aliyezaliwa Miaka 30 iliyopita Mkoani Mara, Elias Selemani Kerenge amesema kitu kingine atakachofanya katika uongozi wake pindi atakapochaguliwa atahakikisha anawasiliana kwa karibu na viongozi wa Umoja huo ngazi ya Taifa ili waweze kuungalia umoja huo hadi katika ngazi ya Wilaya ili kuharakisha shughuli za Maendeleo zilizokusudiwa.