Ebola Sasa ‘Yamfuata’ Obama Marekani

Hospitali ya Presbyterian Jijini Dallas ambapo mgonjwa wa kwanza amegundulika.

Hospitali ya Presbyterian Jijini Dallas ambapo mgonjwa wa kwanza amegundulika.

Ebola Sasa 'Yamfuata' Obama Marekani

Ebola Sasa ‘Yamfuata’ Obama Marekani

IKIWA ni siku chache baada ya Rais wa Marekani, Barrack Obama kutangaza kutoa askari kwenda kusaidia mapambano na ugonjwa wa Ebora katika nchi zenye ugonjwa huo Afrika, Mgonjwa wa kwanza mwenye virusi vya Ebola amegundulika nchini Marekani.

Taarifa zinasema mgonjwa huyo amegundulika akiwa katika Mji wa Dallas, Texas. Maofisa katika kituo cha afya cha Texas Hospitali ya Presbyterian wamesema tayari mgonjwa huyo ambaye hakutajwa jina ametengwa katika hospitali hiyo huku akihudumiwa.

Mgonjwa huyo anasemekana kuwa ni mtu anayeaminika kuambukizwa ugonjwa huo nchini Liberia kabla ya kuonyesha dalili za ugonjwa huo. Zaidi ya watu 3,000 tayari wamefariki dunia kutokana na ugonjwa wa Ebola huko Afrika Magharibi na idadi ndogo ya wafanyakazi wa Marekani wa mashirika ya misaada wamepata nafuu baada ya kupelekwa kutibiwa Marekani.

Jumatatu, maofisa wa kituo cha afya cha Texas katika hospitali ya Presbyterian ya Dallas wamesema mgonjwa ambaye hakutajwa jina alikuwa akichunguzwa virusi vya Ebola na ametengwa katika hospitali hiyo.

Hivi karibuni Rais wa Marekani, Barrack Obama alitangaza mpango wake wa kuwatuma wanajeshi 3,000 Afrika Magharibi kama njia mojawapo ya kusaidia mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ebola. Katika mazungumzo hayo Obama alitoa wito kwa jamii ya kimataifa kuchukua hatua za dharura kuzuia kuenea kwa ugonjwa wa Ebola Magharibi mwa Afrika ambao unaenea kwa kasi sana. Alilisitiza kuwa endapo mlipuko wa maradhi hayo hautodhibitiwa kwa sasa, mamia ya maelfu ya watu wataambukizwa na yatakuwa tishio kwa usalama wa dunia.

Shirika la Afya Duniani, WHO limesema mpaka sasa zaidi ya watu 3,000 wamekufa kutokana na virusi vya Ebola, wengi wa waliokufa ni kutoka Liberia. Nchini Nigeria, nchi yenye idadi kubwa ya watu barani Afrika kuna wagonjwa 19 waliothibitika kuugua ugonjwa wa Ebola na watu wanane wamekufa tangu mgonjwa wa kwanza kuthibitishwa nchini humo mwezi Julai.

Kuna mgonjwa mmoja aliyethibitika nchini Senegal, lakini hakuna taarifa za kifo mpaka sasa. Ebola ni ugonjwa hatari wa virusi kuwahi kuzuka duniani.
-BBC