Ebola Imethibitisha Udhaifu wa Mifumo ya Afya

Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete

Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete


MKUTANO mkubwa wa kimataifa kuhusu masuala ya afya umeambiwa kuwa ugonjwa wa ebola umethibitisha kuwa dunia haijajenga uwezo wa kutosha wa kukabiliana na magonjwa makubwa ya mlipuko.
Aidha, mkutano huo uliofanyika, Januari 27, 2015, katika mji mkuu wa Ujerumani wa Berlin, umeambiwa kuwa ugonjwa huo wa ebola umethibitisha kuwa mifumo wa afya ya umma kwa baadhi ya nchi bado ni dhaifu mno kukabiliana na magonjwa ya mlipuko.

Hayo yameelezwa katika mkutano wa kimataifa wa kujadili na kuchangia upya juhudi za kimataifa za taasisi ya Global Alliance for Vaccines and Immunisation (GAVI) ambayo imefanya kazi kubwa ya kusambaza chanjo duniani ambapo mpaka sasa watoto milioni 500 wamepata chanjo za kuzuia magonjwa mbali mbali na wengine milioni saba wameokolewa katika hatari ya kupoteza maisha.

Katika mkutano huo ambako Bara la Afrika linawakilishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete na Rais wa Mali, Mheshimiwa Babacar Keita, Kiongozi wa Ujerumani, Kansela Angela Merkel amesema kuwa ugonjwa wa ebola umesumbua sana dunia kwa sababu dunia haijajenga uzoefu na uwezo wa kutosha kukabiliana na magonjwa makubwa ya mlipuko.

Kansela Merkel amewaambia mamia ya wajumbe wa mkutano huo kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Berlin Congress Centre: “Ugonjwa wa ebola umethibitisha kuwa tunahitaji katika muda wa kati na mfupi, kuimarisha mifumo yetu ya afya kuweza kukabiliana ipasavyo na magonjwa ya milipuko.”

Naye Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Bwana Donald Kaberuka ameuambia mkutano huo kuwa ugonjwa wa ebola umethibitisha jinsi gani dunia na hasa nchi zinazoendelea hazina uwezo wala maandalizi ya kukabiliana na magonjwa makubwa ya mlipuko.

“Ugonjwa wa ebola umethibisha ukweli huu. Ebola haukuwa ugonjwa tu wa kawaida lakini pia ugonjwa huo umeonyesha udhaifu wa mifumo ya afya ya umma katika nchi mbali mbali,” amesema Dkt. Kaberuka ambaye alikuwa mmoja wa wazungumzaji katika mkutano huo.

Mwaka jana, ugonjwa wa ebola uliua mamia kwa mamia ya wananchi katika nchi za Afrika Magharibi zikiwemo Sierra Leone, Liberia, Mali, Guinea na Nigeria.