MFANYAKAZI wa Shirika la madaktari la Medecins Sans Frontieres (MSF) nchini Liberia amesema hawezi kuusahau ugonjwa wa Ebola maishani kwake kwa kile kuteketeza familia yake. Kwa sasa mfanyakazi huyo tayari ametenganishwa na familia yake kutokana na kazi yake, habari hizo zilikuwa ni vigumu kuvumilia kwa namna zilivyomuumiza.
Lakini aliokolewa katika hali ya kuchanganyikiwa baada ya kusikia mtoto wake wa kiume mwenye umri wa miaka 18 ambaye alikuwa mtu wa 1,000 kutibiwa na taasisi moja ya kujitolea kupona maambukizi ya virusi vya Ebola.
Tarehe 21 Septemba, ni siku ambayo sitaweza kuisahau: Nilikuwa nje nikifanya kazi na shirika la MSF kama afisa uenezi wa afya, nikitembelea vijiji na kuwaambia watu juu ya Ebola. Nikapata simu kutoka kwa mke wangu. Nikajibu simu hiyo lakini hakuna mtu aliyeongea.
Alikuwa akiishi katika mji mkuu wa Monrovia, na watoto wetu watatu, wakati mimi nikiwa nafanya kazi Foya, kaskazini mwa Liberia. Wakati huo Ebola ilikuwa imeingia Liberia kwa hiyo nikajaribu kuzungumza na familia yangu juu ya virusi vya Ebola na kuwaelimisha, lakini mke wangu hakuamini.
Nilimpigia simu mke wangu nikimtaka kuondoka Monrovia na kuwaleta watoto kaskazini, hakusikia, alipinga kuwepo kwa Ebola. Baadaye usiku huo, kaka yangu alinipigia simu: “Mke wako amekufa.” Alexander Kollie aliyepoteza karibu familia yake yote kutokana na Ebola nchini Liberia. Nilisema: “Nini?” Alisema: “Bendu amekufa.” Nilidondosha simu; Niliitupa mbali na ikavunjika vipande. “Hakuwa na dalili yoyote ya kutapika au kuharisha, lakini alionekana kuchoka,” Alexander Kollie.
Tulikuwa pamoja kwa miaka 23. Ni yeye peke yake aliyeelewa fika maisha yangu. Nilihisi kwamba nilipoteza kumbukumbu yangu yote. Macho yangu yalikuwa wazi, lakini sikujua nilikuwa naangalia nini, Sikuwa naona. Baadaye wiki hiyo hiyo, nilipata simu nyingine kutoka Monrovia. Kaka yangu, ambaye alikuwa akifanya kazi ya uuguzi, alikuwa akimhudumia mke wangu.
Halafu watoto wangu wawili wadogo walichukuliwa kwenda kituo cha matibabu mjini Monrovia, lakini mabinti zangu walikuwa wanaumwa na walikufa. Alexander Kollie akiwa katika kituo cha kuhudumia wagonjwa wa Ebola. Nilijisikia kukosa zaidi msaada; Nilikuwa nachanganyikiwa; Sikuwa na uelewa wa jambo lolote.
Mtoto wangu mkubwa wa kiume, James Kollie – ambaye pia anajulikana kama Kollie – alikuwa bado Monrovia katika nyumba ambayo familia yetu ilikuwa ikiugulia, japokuwa hakuonyesha dalili za ugonjwa. Alinipigia simu na kusema: “Kila mtu ameugua, Sijui nini cha kufanya.” Nilimwambia aje huku Foya akae nami.
Wakati kijana wangu alipowasili, watu kijijini hapa hawakutukubali. Walituambia kuwa familia yetu wote wamekufa na nimwondoe Kollie. Nilichukizwa na kauli zao. Nilijua hakuwa na dalili zozote na hakuwa kitisho kwao lakini kwa sababu ya unyanyapaa hawakutaka tukae hapo. Ikabidi tuendelee. Siku ya pili, japo nilibaini kuwa kijana wangu alikuwa amechoka zaidi ya kawaida yake, niliingiwa na woga juu yake.
Alexander Kollie aliweza kumtembelea mtoto wake katika kituo cha kuwatibu wagonjwa wa Ebola. Hakuwa na dalili zozote za Ebola kama kutapika au kuharisha, lakini alionekana kuchoka. Nilipiga simu ya mawasiliano kuhusu Ebola na MSF walimpeleka katika kituo cha wagonjwa wa Ebola hapa Foya ili kupimwa.
Wakati majibu yalipotoka na kuonya ana maambukizi ya Ebola, ulikuwa usiku wa mateso kwangu. Usiku mzima nilikuwa nalia na kufikiria kile ambacho kingempata mtoto wangu. “Acha kulia baba… Dada zangu wamekufa, lakini nitapona na nitakufanya uwe na furaha,” James Kollie.
Siku iliyofuata, washauri nasaha wa MSF walinituliza. Waliniambia nisubiri. Kubaki na amani. Nilikaa pamoja nao na kuzungumza kirefu. Niliweza kumwona mwanangu katika kituo cha matibabu kupitia uzio, na nilimwita: “Mwanangu, wewe ni tumaini langu pekee. Jipe moyo. Dawa yoyote watakayokupa, unatakiwa kutumia.”
Aliniambia: “Baba, Najua. Nitafanya hivyo. Acha kulia baba… Dada zangu wamekufa, lakini nitapona na nitakufanya mwenye furaha.” Kila siku washauri nasaha walihakikisha wananiona, na walikaa pamoja nami ili niweze kuzungumza. James Kollie akiwa na uso wa furaha baada ya kuambiwa amepona Ebola. Baada ya muda fulani mtoto wangu alianza kuimarika. Alikuwa akitembea tembea hapo lakini nilikuwa na wasiwasi nilipoona kuwa macho yake bado ni mekundu.
Halafu kitu chakushangaza kilitokea, kitu ambacho kwa kweli sikuamini mpaka nilipoona. Nimeona watu wenye Ebola wakianza kuonekana wenye nguvu na halafu siku inayofuata wanatoka. Kwa hiyo pia nilikuwa nafikiria, huenda mtoto wangu akawa mmoja wa wale watakaotoka siku inayofuata.
Hatimaye wakati nilipomwona anatoka nje, Nilijawa na furaha sana sana. Nilimwaangalia na aliniambia: “Baba, ni mzima.” Nilimkumbatia. Watu wengi walikuja kumwona akitoka nje. Kila mtu alijawa na furaha alipomwona akitoka. Halafu MSF waliniambia, huyo ni mgonjwa wa 1,000 katika kituo hicho kunusurika kutokana na ugonjwa wa Ebola.
James Kollie, mwenye umri wa miaka 18, anataka kusoma baiolojia na kuwa daktari. Hili jambo kubwa, lakini nilikuwa nashangaa, ni watu wangapi tumewapoteza? Lakini nina furahi sana kumwona Kollie amepona, lakini ni vigumu kutowafikiria wale tuliowapoteza. Nilipomchukua na kurejea naye nyumbani, kwa kweli alikuwa na uso wenye tabasamu. Nami pia, nilikuwa na tabasamu kubwa usoni pangu.
Niliamua kumfanyia tafrija ndogo. Tangu wakati huo, tulifanya kila kitu pamoja. Tulilala pamoja, tunakula pamoja na tumekuwa tukizungumza sana. Nilimwuliza: “Malengo yako ni nini baada ya kuhitimu sekondari?” Ni mwanafunzi wa darasa la kumi. Aliniambia anataka kusoma baiolojia na kuwa daktari. Kwa sasa nitajaribu kila njia kutimiza malengo yake na kufanikiwa katika maisha, ili asiumie sana juu ya mateso aliyopata ya kumpoteza mama yake.
Nilimwaambia: “Kwa sasa mimi ni baba yako na mama yako. Nakufanyia yote kwa sasa.” Ana umri wa miaka 18 sasa, kwa hiyo nitamfanya rafiki yangu… kwa sababu ni mtu peke ambaye naweza kuzungumza naye. Siwezi kupata mke mbadala, lakini naweza kuanza maisha mapya na mtoto wangu.
-BBC