EAC Yazindua Utafiti wa Uelewa wa Raia Kuhusu Mtangamano

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Dk. Richard Sezibera

Na Mwandishi wa EANA, Arusha

KATIBU Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Dk. Richard Sezibera ameelezea umuhimu wa kuifanya jumuiya hiyo kuwa yenye msisimko zaidi na ya kuvutia.

“Jumuiya yetu (EAC) inatakiwa kuwa ya manufaa, yenye ufanisi, msisimko na ya kuvutia kuwawezesha wana Afrika Mashariki kupata kilichobora kutoka kwake,” alisema katika makao makuu ya jumuiya hiyo Jijini Arusha, Shirika Huru la Habari la Afrika Mashariki (EANA) linaripoti.

Dk. Sezibera alikuwa anazindua utafiti juu ya uelewa wa raia wa Afrika Mashariki kuhusu mtangamano wa Jumuiya hiyo, unaofanywa kwa ushirikiano baina ya EAC na Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Ujerumani (GIZ) katika nchi tano wanachama wa jumuiya hiyo.

Halfla hiyo ya muda mfupi alihudhuriwa na Timu ya Watafiti na maafisa waandamizi wa GIZ, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na EAC. Utafiti huo utakaofanywa katika nchi wanachama ambazo ni Burundi, Kenya, Rwanda, Tanzania na Uganda utachukua mwezi mmoja na unatarajiwa kumalizika Agosti 24.

Utafuti huo utafanyika kwa njia ya madodoso ya kwenye mtandao na kwa mahojiano ya moja kwa moja katika maeneo maalum yatakayochagulia kwenye majiji na miji ya mipakani. 

“Utafiti huo unatarajiwa kutupatia mwanga juu ya namna ya watu wanavyoiona EAC, wanaifahmu vizuri kiasi gani, jinsi wanavyozifahamu nembo za EAC na jinsi wavyoitathmini utendaji wake,” aliongeza.

Kwa mujibu wa taarifa ya EAC, kubwa zaidi katika utafiti huo ni kutathmini jinsi taarifa zinavyowafikia walengwa na jinsi inavyoeleweka na raia wa Afrika Mashariki na namna gani ya kuweza kusonga mbele.

Dk. Sezibera alizipongeza juhudi hizo za utafiti, akisema zipo katika uhalisia wa kutaka kuileta jumuiya hiyo karibu zaidi na walengwa.

Mkuu wa Mawasiliano na Masuala ya Umma wa EAC, Owora Richard Othieno alisema kuwa mradi huo unalenga kubaini kama ndoto za mtangamano za wana Afrika Mashariki zinaendana na matakwa ya Mkataba wa EAC.