Na Mtuwa Salira, EANA, Arusha
KATIBU Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Dk Richard Sezibera ametoa wito kwa waandishi wa habari katika kanda hiyo kuripoti habari chanya juu mwenendo wa mtangamano wa jumuiya hiyo.
“Muwe mstari wa mbele katika kuripoti kwa uhakika juu ya mtangamano wa EAC, manufaa yake mengi na fursa za kutosha zilizopo kwa watu wa kanda hii na kwa manufaa ya wote,” Dk Sezibera aliwaambia waandishi wa habari wapatao 15 na wahariri waliokuwa wanahudhuria mkutano wa wiki moja juu ya namna ya kuripoti migogoro baina ya dini mbalimbali, mjini Kigali, Rwanda juzi.
Mafunzo hayo yanaenda sambamba na mkutano wa siku tano wa ushirikiano baina ya dini mbalimbali ili kuimarisha amani na usalama EAC. Kiongozi huyo wa ngazi ya juu wa EAC alisema jukumu la vyombo vya habari katika mtangamano wa EAC liwe ni kubadilisha mawazo mgando ya watu ili kupokea kwa urahisi na kwa furaha mwenendo mzima wa ushrikiano.
“Lakini ili kutekeleza hilo nyinyi wenyewe hamnabudi kuwa na fikra chanya kuhusu mtangamano na kwa kufanya hivyo mtaweza kuona na kuandika kwa mawazo chanya kuhusu kanda yetu,” alisisitizaz Dk Sezibera katika taarifa kwa vyombo vya habari.
Vyombo vya habari na wahariri, aliongeza, vina nafasi maalum kuimarisha mtangamano kwa kuandika kwa ukweli bila kupendelea kazi nyingi zinazofanywa na EAC katika nchi wanachama.
“Ni muhimu sana kwa waandishi wa habari wa EAC kuhakikisha kwamba wanasaidia katika kuimarisha maleno ya jumuiya,” alisema.
Mafunzo hayo yaliendeshwa na waandishi wa habari wagongwe na washauri wa mambo ya habari ikiwa ni pamoja na Dk Christopher Kayumba kutoka Rwanda na Dk. Haron Mwangi wa Kenya.