EAC Yaonguza Kupunguza Migogoro katika Nchi zake

EAC
Na James Gashumba, EANA

Nchi tatu za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) za Rwanda, Burundi na Tanzania zimetajwa kuwa ni miongoni mwa nchi zilizofanikiwa kuharakisha kwa kasi kubwa kukua kwa maendeleo endelevu ya binadamu kwa kupunguza migogoro na kujenga ushupavu baina ya raia wake kati ya mwaka 2000 na 2013.

Taarifa ya hivi karibuni iliyotolewa na Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) imeonyesha kwamba Rwanda ipo katika ngazi moja na Ethiopia katika bara la Afrika ikifuatiwa na Burundi,Msumbiji,Tanzania na Zambia.

Taarifa imefafanua kwamba Afrika inafurahia kiwango cha juu cha kukua kwa uchumi na ubora wa maisha lakini ukosefu wa usalama na majanga ya asili na yanayoletwa na binadamu yanazidi kushamiri katika kanda.

‘’Kukabiliana na migogoro na kuwalinda wanaothirika vibaya na migogoro hiyo,ni jambo la msingi ili kuhakikisha kunakuwapo maendeleo endelevu kwa waliowengi,’’ alisema Mkurugenzi wa UNDP Kanda ya Afrika, Abdoulaye Mar Dieye.

Alizitaka nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara kuimarisha vita dhidi ya migogoro ili kulinda maendeleo yaliyokwishapatikana kuepuka kurudishwa nyuma.

Taarifa hiyo imetaja baadhi ya vingengele vinavyohitajika ili kuyalinda mafanikio yalikwisha patikana katika kanda hiyo kuwa ni pamoja na ajira, hifadhi ya jamii na kuwa na jamii imara.

Imefafanua kwamba kudhibiti mitikishiko ya migogoro na kukuza fursa kwa wote kunaweza kusadia kwa kiasi kikubwa kupunguza uwezekano wa kuibuka kwa migogoro mingine na kujenga ushupavu.

Naye Afisa Rasilimali Watu wa UNDP, Helen Clark alisema kuondoa umasikini siyo tu kunahusu ‘kufikia kiwango cha sifuri’ lakini pia ni pamoja kubaki katika kiwango hicho.