Na Denis Bizimana, EANA
Mpango wa kanda wa kuelimisha jamii kufahamu faida na fursa zilizopo katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwa wananchi wanaoishi maeneo ya mipakani, umeanza katika mji wa Rusumo,mpakani mwa Tanzania na Rwanda.
Lengo kuu la mpango huo ni kuongeza kiwango cha uelewa wa wananchi wanaoshi mipakani juu ya umuhimu wa uwepo wa jumuiya hiyo na pia kwa wafanyabiashara ndogondogo kupata uelewa wa fursa zilizopo za mtangamano, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari juzi, Shirika Huru la Habari la Afrika Mashariki (EANA) linaripoti.
Akizungumza kwa niaba ya Afisa Uhusiano Mwandamizi wa EAC,Mtaalamu wa Masuala ya Habari EAC na Shirika la Misaada la Ujerumani (GIZ), Sukhdev Chhatbar alisisitiza umuhimu wa kuwawezesha wananchi wa kawaida kufahamu vyema jumuiya ili waweze kushirika kikamilifu katika suala zima la mtangamano.
Aliongeza;”Ipo haja ya kuhakikisha kwamba raia wa EAC wanawezeshwa kupata taarifa na ufahamu wa kutosha ili kushiriki kikamilifu katika mwenendo mzima wa mtangamano wa jumuiya yao na kushiriki katika kuleta maendeleo katika kanda.”
Mada mbalimbali ziliwasilishwa kwa wananchi waliohudhuria warhsa hiyo ya uhamasishaji wa uelewa ikiwa ni pamoja na Umoja wa Forodha na Soko la Pamoja,faida zake, mahitaji na utaratibu wa kupata hati za kuweza kusafiri na kusafirisha bidhaa,huduma,mitaji na kazi katika vituo vya mipakani.
Warsha hiyo pia imehudhuriwa na maafisa kutoka wizara zinazoshughulika na masuala ya EAC kutoka Rwanda na Tanzania.
Mafunzo hayo kwa raia wa mipakani yametolewa na Balozi wa Vijana EAC,Raymond Maro ikiwa ni sehemu ya mpango huo wa uhamasisha.
Warsha ijayo ya uhamasishaji imepangwa kufanyika katika miji ya Manyovu nchini Tanzania na Mugina nchini Burundi wiki ijayo.