EAC yaahidi kukabiliana na uhalifu wa mitandao

Nembo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki

Na James Gashumba, EANA-Arusha

AFRIKA Mashariki inafuatilia kwa kasi utekelezaji wa juhudi za kudhibiti changamoto ya uhalifu wa njia za mtandao unaotumika mipakani na ambao unatishia amani na utulivu katika kanda hiyo.

Maofisa wa serikali wanasema, kanda ya Afrika Mashariki iko katika hatari ya kukumbwa na uhalifu mbalimbali unatumika kwa njia ya mitandao ikiwa ni pamoja na uhalifu wa fedha, madawa ya kulevya, usafirishaji binadamu na ugaidi.

“Kuna haja ya kuandaa mkakati wa pamoja kushughulikia usalama wa mitandao. Kama kanda hatuna budi kuanza kushirikiana kukabiliana na tishio la usalama wa mitandao katika ngazi za kitaifa na kikanda,” Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari wa Kenya, Bitenge Ndemo alisema katika Jukwaa la Uendeshaji Mitandao la Afrika Mashariki, mjini Nairobi, Kenya.

Mataifa ya Afrika Mashariki yameongeza juhudi za kupambana na uhalifu unaotokana na mitandao ya mawasiliano kwa kushirikisha wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na serikali, wadau katika sekta hiyo na asasi za kiraia.

“Kenya ina kamati ya kitaifa ya kushughulikia usalama wa mitandao chini ya Tume ya Mawasiliano ya Kenya (CCK). Vyombo vya dola vinavyosimamia utekelezaji wa sheria pamoja na wadau katika sekta hiyo wanajumuishwa katika juhudi hizo,” alisema Ndemo.

Kwa mujibu wa Ndemo, kamati ya muda ya kushughulikia usalama wa mitandao chini ya uenyekiti wa Kenya imekuwa ikiratibu shughuli zote zinazolenga kudhibiti uhalifu wa kwenye mitandao katika nchi zote tano wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki za Kenya, Uganda, Tanzania, Rwanda na Burundi.

Naye Rais wa Chama cha Mtandao wa Intaneti nchini Rwanda, Chris Mulola alidokeza juu ya utafiti uliofanywa na taasisi moja ya kimataifa ijulikanayo Deloitte and Touche ambayo imebaini kwamba asilimia 60 ya benki za Afrika Mashariki zipo katika hatari ya kukumbwa na uhalifu wa kwenye mitandao ya mawasiliano.

Ghama za jumla zilizokadiriwa kuwa ni tishio la uhalifu huo kwa taasisi za fedha katika kanda hiyo umefikia dola za kimarekani milioni 245. Molola ametoa wito wa kuanzishwa kwa vyombo vya kusimamia na kutoa taarifa za uhalifu wa kwenye mitandao katika mipaka yote.