EAC Wakubaliana Mgawanyo wa Vituo vya Mafunzo ya Polisi

IGP Said Mwema Akikagua gwaride

By James Gashumba, EANA

Wakuu wa majeshi ya polisi ya nchi wanachama za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wamekubaliana kuanzisha vituo mbalimbali vya mafunzo vyenye ubora katika kanda ili kuvijengea uwezo wa kukabiliana na changamoto mbalimbali.

Vituo hivyo vitajikita katika masuala mbalimbali yakiwemo ya unyanyasaji wa kijinsia, udhibiti wa majanga, uchunguzi wa makosa ya jinai,udhibiti wa silaha haramu na utii wa sheria.

Vituo hivyo vitatoa mafunzo mbalimbali kwa maafisa wa majeshi ya polisi wa nchi za EAC kwa lengo ya kuwajengea uwezo kiutendaji.

Mkutano wa wakuu wa majeshi ya polisi uliofanyika Kampala, Uganda mwishoni mwa wiki umekubaliana kwamba nchi hiyo iwe mwenyeji wa Kituo cha Polisi Jamii huku Rwanda kuwa Kituo cha Mafunzo na Udhibiti wa Unyanyasaji Kijinsia.

”Dhana hiyo inahusu yule mwenye msingi mzuri katika nyanja fulani ambako sote ndiko tunaweza kuanzia,” Mkuu wa Jeshi la Polisi la Uganda (IGP), Kale Kayihura alieleza.

Mratibu wa Polisi wa Rwanda wa Masuala ya Uchunguzi wa mwili wa Binadamu,Wilson Rubanzana alisema moja ya vituo hivyo kitakuwa makao makuu ya Jeshi la Polisi mjini Kigali nchini mwake.

Alisema vituo vingine vitakuwa katika Chuo cha Taifa cha Polisi cha Musanze,Kaskazini ya Rwanda na Chuo cha Mafunzo ya Polisi, Mashariki mwa Rwanda.

Mkutano huo pia uliichagua Kenya kuwa kituo cha masuala ya Anga na Makosa ya Jinai wakati Tanzania itakuwa mwenyeji wa kituo cha Polisi wanamaji na Udhibiti wa Sheria.

Burundi kutokana na uzoefu wake wa masuala ya kushughulika na migogoro itakuwa mwenyeji wa kituo cha Udhibiti wa majanga na silaha haramu.

Uganda kwa upande wake itakuwa mwenyeji wa kituo cha Uchunguzi wa mwili wa binadamu.