EAC na msimamo wa biashara za silaha duniani

Na mwandishi wetu

WATAALAMU wa masuala ya usalama toka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wanakamilisha maandalizi ya msimamo wa pamoja wa kikanda utakaowasilishwa mwezi ujao katika mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mkataba wa Biashara ya Silaha (AAT) mjini New York, Marekani.

Mratibu wa Kitaifa wa Masuala ya Silaha Ndogondogo nchini Uganda, Ahmed Wafuba alisema hatua hiyo itasaidia juhudi za kanda katika mapambano yake dhidi ya silaha haramu ambazo ni chanzo cha upotevu wa maisha ya watu wasiokuwa na hatia.

‘’ Tumeshafikia maafikiano juu ya suala hili na kinachobakia ni kuupeleka kwenye Baraza la Mawaziri,’’ Wafuba aliliambia Shirika Huru la Habari la Afrika Mashariki (EANA) wakati wa kuzindua wiki ya dunia ya mapambano dhidi ya matumizi ya bunduki katika ghasia, mjini Kampala, Uganda mapema wiki hii.

Wiki hiyo ya uhamasishaji imeratibiwa na Sekretarieti ya EAC kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) na taasisi ya East African Action Network on Small Arms (EAANSA).

Wafuba alisema kwamba nchi wanachama wa EAC zitaunga mkono Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Biashara ya Silaha ambao ndiyo chombo pekee cha kisheria kinachosimamia viwango vya juu vya kimataifa vya usafirishaji wa silaha.

‘’Suala la silaha za kawaida na silaha ndogondogo pamoja na milipuko hazina budi kudhibitiwa kisheria,’’ alisema na kuongeza kwamba Uganda kwa upande wake umeshateketeza silaha 97,000 katika kipindi cha miaka mitatu.

Mataifa mengi yameelezea wasiwasi wao juu ya kutokuwepo kwa sheria na taratibu zinazokubalika na nchi zote duniani katika udhibiti wa usafirishaji wa silaha.

Akitoa mfano wa Mrusi mmoja anayejulikana kwa jina la Viktor Bout, maarufu kama ‘’Mfanyabiashara wa Kifo’’, Waziri wa Nchi wa Uganda wa Masuala ya Mambo ya Ndani, James Baba alitaka mkataba huo kuwazuia watengenezaji wa silaha kuwauzia silaha hizo wahalifu.

‘’Watu wetu hawauawi kwa vifaru au silaha nyingine hatari bali wanauawa na silaha ndogondogo zinaosambazwa na wafanyabiashara wa kifo,’’ alisema Baba.

Naye Martin Oganda, afisa wa GIZ-SALW anayeshghulikia masuala ya kuhamasisha amani na usalama alishangaa kubaini kwamba mpaka sasa hakuna sheria ya dunia inayodhibiti usafirishaji wa silaha kutoka kwa watengenezaji hadi kwa mtumiaji.

Mkutano huo wa Umoja wa Mataifa juu ya Mkataba wa Biashara ya Silaha utafanyika kati ya Julai 2 na 27, 2012.