Dunia Yamuaga Mandela kwa Heshima ya Kipekee, Zaidi ya Viongozi 100 Mashughuli Wahudhuria..!

Dunia Yamuaga Mandela kwa Heshima ya Kipekee

Dunia Yamuaga Mandela kwa Heshima ya Kipekee

DUNIA imeamua kumpa heshima ya kipekee Nelson Mandela kwa kufanya mkusanyiko wa aina yake wa kumuaga kwenye kitongoji cha Soweto, ambapo zaidi ya viongozi 100 wa dunia wamehudhuria ibada hiyo. Heshima kubwa kupita kiasi ameandaliwa Hayati Nelson Mandela, mmojawapo wa vigogo vya karne ya 20, ambapo umati mkubwa wa aina ya pekee wa viongozi wa mataifa na serikali unakusanyika kuungana na Waafrika ya Kusini leo katika uwanja wa michezo mjini Soweto, katika sala maalum ya kumuombea hayati Mandela kabla ya kuzikwa Jumapili ijayo.

Tangu walioko madarakani mpaka waliostaafu, katika tukio la kihistoria ambalo halijawahi kushuhudiwa huku zaidi ya watu 95, 000 wakifurika uwanjani tangu usiku wa manane kuhakikisha wanapata nafasi. Kitongoji hicho cha Jonnesburg ndiko alikokuwa akiishi Mandela kabla ya kukamatwa na kuwekwa gerezani kwa miaka 27, kwa hivyo ni mahala pa kihistoria kutoa heshima za mwisho kwa shujaa huyo wa mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi, kwa sababu eneo hilo ni kitambulisho cha kutengwa makusudi kwa Waafrika ya Kusini weusi na wale weupe waliokuwa wakiishi Johannesburg.

Kiasi cha viongozi 100 wanahudhuria, wakiwemo wa mataifa na serikali, wafalme au warithi ufalme bila ya kuwahesabu watu wengineo mashuhuri duniani ikiwa ni pamoja na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Afrika, Nkosazana Dlamini Zuma, na wajumbe wa Baraza la Wazee la Kimataifa aliloliunda mwenyewe Nelson Mandela, akiwemo rais wa zamani wa Marekani, Jimmy Carter.

Marekani inawakilishwa na Rais Barack Obama na mkewe pamoja na marais wa zamani, George W. Bush na Bill Clinton na mkewe, waziri wa zamani wa mambo ya nchi za nje, Hillary Clinton. Viongozi wengine ni pamoja na Rais Raul Castro wa Cuba, Hamid Karzai wa Afghanistan, Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron, na Mwanamfalme Charles, Rais Pranab Mukhrejee wa India, Rais Dilma Russels wa Brazil na watangulizi wake wanne ikiwa ni pamoja na Lula da Silva, Waziri mkuu wa Italia Enrico Letta, Kiongozi wa Mamlaka ya Utawala wa Ndani wa Palestina, Mahmoud Abbas na pia mawaziri wakuu wa Norway, Sweden na Canada, kwa kuwataja wachache tu.

Jamhuri ya Umma wa China inawakilishwa na Makamo wa Rais Li Yuanchao huku Japan ikiwakilishwa na mrithi wa kiti cha mfalme, Mwanamfalme Naruhito. Ujerumani inawakailishwa na Rais Joachim Gauck. Takriban viongozi wote wa bara la Afrika wanahudhuria pia ibada hiyo.

Ibada kadhaa nyengine zinafanyika hadi siku ya mazishi ya Mandela katika kijiji walichotokea wazee wake, Qunu, Desemba 15. Mbali na ibada rasmi ya mazishi hii leo, maiti ya Nelson Mandela itawekwa katika Ikulu kuanzia Jumatano hadi ijumaa itakaposafirishwa kwa ndege hadi Mashariki ya Cape Town kwa mazishi. Hatua za ulinzi zimeimarishwa. Afrika kusini inauzoefu kutokana na maandalizi ya Kombe la Dunia la Dimba mwaka 2010. Waziri wa Ulinzi, Nosiviwe Mapisa-Nqakula, amesema,”Kila kitu kiko tayari, tumejiandaa tangu miaka mitatu au minne iliyopita.”