Na Mwandishi Wetu
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete ameuangiza uongozi wa Soko la Mitaji na Hisa la Dar es Salaam (DSE) kuchukua hatua za haraka kufungua milango ili Watanzania wengi zaidi wajiunge kuwa wanachama wa soko hilo badala ya idadi ya sasa ya wanachama 37 tu. DSE ilianzishwa kwa mtaji wa umma na ni mali ya Serikali.
Aidha, Rais Kikwete ametaka kuona kasi zaidi katika maandalizi ya kuanzishwa kwa soko la mitaji na mazao nchini kama njia ya uhakika zaidi ya kuwalinda wakulima wadogo dhidi ya walanguzi wa mazao ambao wanawalipa wakulima kiasi kidogo cha fedha.
Rais Kikwete ametoa maagizo hayo Alhamisi, Mei 10, 2012, wakati alipotembelea na kupewa maelezo kuhusu uendeshaji wa Soko la Mitaji na Mazao la Ethiopia – Ethiopia Commodities Exchange (ECX) mjini Addis Ababa ambako Rais Kikwete alikuwa anahudhuria Mkutano wa Jukwaa la Uchumi Duniani (World Economic Forum), Kanda ya Afrika uliomalizika leo, Ijumaa, Mei 11, 2012.
Wakati wa ziara hiyo, Rais Kikwete aliuliza kuhusu maendeleo na idadi ya wanachama wa DSE baada ya kuambiwa kuwa ECX lilioanzishwa miaka minne tu iliyopita limefanikiwa kufikisha wanachama 450 katika kipindi kifupi.
Baada ya kuambiwa kuwa DSE ina wanachama 37 tu baada ya kuwa imeanza na wanachama saba, Rais Kikwete alionyesha kushangazwa na idadi hiyo na aliangiza: “Hii ni hali isiyokubalika. Hii ni taasisi ya umma haiwezi kuendelea kufunga milango kwa watu wengi zaidi na kunufaisha wanachama 37 tu. Nataka kuona hali hii ikibadilishwa katika kipindi kifupi.”
Baada ya kupewa maelezo ya kina na ufasaha na Dkt. Eleni Z Gabre-Madhin, Mtendaji Mkuu wa ECX, kuhusu historia ya uendeshaji wa soko hilo, Rais Kikwete aliagiza watendaji wa Serikali wanaosimamia mchakato wa kuanzishwa kwa soko kama hilo nchini kuongeza kasi kwa sababu soko la namna hiyo ni mkombozi mkubwa wa mkulima.
“Hakuna shaka kuwa soko kama hili litakuwa na faida kubwa katika maendeleo ya kilimo ya wananchi wetu. Ni lazima tulianzishwa haraka iwezekanavyo. Tunahitaji soko yenye utulivu na uhakika kwa ajili ya wakulima wetu. Hii ndiyo njia pekee ya kuwalinda wakulima wetu dhidi ya mkulima mdogo anayeendelea kuteswa na mlanguzi na mchuuzi wa mazao katili na asiyekuwa na huruma kabisa.”
Dk. Gabre-Madhin alimweleza Rais Kikwete kuwa ni mazao manne ambayo kwa sasa yanachuuzwa kwenye ECX ambayo ni kahawa, ufuta, mahindi na njegere. “Mheshimiwa Rais sasa hakuna tena ulanguzi wa mazao haya katika Ethiopia kwa sababu bei ya kila zao ni moja katika pembe zote za nchi yetu na wakati wowote. “
Aliongeza mama huyo: “Kama unavyojua Mheshimiwa Rais mkopeshaji mkubwa katika Afrika siyo Benki ya Dunia ama Shirika la Fedha Duniani (IMF) bali ni mkulima mdogo ambaye hutoa mazao yake kwa mikopo kwa watu mbali mbali. Soko hili limemaliza mikopo hiyo. Sasa mkulima wa Ethiopia hakopeshi tena na kila saa tano ya asubuhi ya kila siku, fedha za mazao yake anayoyauliza siku hiyo inakuwa tayari kwenye akaunti yake ya benki.”