Na Mwandishi Wetu, Dodoma
NAIBU Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Dk. Asha-Rose Migiro, Agosti 10, 2011 anatarajia kuzindua ripoti mpya ya Mpango wa Bara la Afrika Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM).
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na Katibu Mtendaji wa APRM Tanzania, Rehema Twalib, ripoti hiyo itakayoonesha Hali ya Utawala Bora nchini kwa mujibu wa maoni ya wananchi na wataalamu mbalimbali. Ripoti pia itajumuisha ile ya awali ya mwaka 2009 kwa nia ya kuongeza takwimu mpya kutokana na mabadiliko mbalimbali yaliyokwishajitokeza katika kipindi cha Julai mwaka huo hadi sasa.
Aidha baada ya uzinduzi huo, wadau zaidi ya 100 wa masuala ya utawala bora nchini watashiriki katika semina ya siku moja ya kuihakiki ripoti hiyo ambapo watafiti walioshiriki kukusanya maoni wataeleza mambo yaliyobainika katika utafiti wao wa hali ya utawala bora nchini na kisha kuwapa wadau hao fursa ya kutoa maoni ili kuiboresha zaidi ripoti hiyo.
Kabla ya kuteuliwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kushika wadhifa alionao sasa, Dk. Migiro alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, wadhifa uliompa fursa ya kuusimamia mchakato huu wa APRM kwa karibu.
Utafiti wa APRM umehusisha wataalamu hao kuangalia maeneo makuu manne ambayo ni demokrasia na utawala bora katika siasa; utawala bora katika mashirika ya umma; utawala bora katika uendeshaji wa makampuni na mwisho wamepitia namna nchi inavyowajibika katika utoaji wa huduma za kiuchumi na kijamii.
APRM ni mpango endelevu uliobuniwa na marais wa Afrika katika kikao chao cha mwaka 2002 ambapo walikubaliana kuweka utaratibu wa kila nchi kuanzisha taasisi hiyo na kisha kuipa jukumu la kufanyakazi ya kujitathmini mara kwa mara katika nyanja za utawala bora.
Mkataba huo wa Afrika unaonesha kuwa nchi hufanyiakazi changamoto zilizobainishwa kwa kutekeleza Mpangokazi kwa miaka mitatu na nchi husika pia itatahminiwa upya kiutawala bora kila baada ya miaka minne. Tayari nchi kadhaa za Afrika za Kenya, Rwanda na Ghana, zilikwishafanya hivyo na sasa zinarudia tena utafiti huo kwa mara ya pili ili kubaini changamoto mpya na kuzifanyikakazi.