Na Joachim Mushi
HATIMAYE kampuni ya kuzalisha umeme ya Symbion ya nchini Marekani imetamka rasmi kuwa tayari imenunua mitambo ya kufua umeme ya kampuni ya Dowans iliyopo eneo la Ubungo jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Meneja Mtendaji wa Symbion, Paul Hinks (pichani juu akiwa na Mwenyekiti wa Symbion, Balozi mstaafu Joseph Wilson) amethibitisha tayari kampuni hiyo imekwisha tiliana saini katika mikataba ya ununuzi wa mitambo hiyo.
Hata hivyo alisema hayupo tayari kutaja kiasi cha fedha ambacho wamelipa katika ununuzi wa mitambo hiyo kwani ni siri kati yao na kampuni ya Dowans kwa mujibu wa mkataba wao.
“Mazungumzo na Dowans yalikuwa ni magumu hasa ukizingatia historia ya mradi wenyewe. Kwa hiyo ilibidi kufanya uchunguzi wa kina kujiridhisha na kila kipengele cha makubaliano na pia ubora wa mitambo na tumejiridhisha kuwa mitambo hii iko katika hali nzuri ya matunzo,” alisema Hinks akiwaeleza wanahabari.
Aidha Hinks aliendelea kusema; “nafarijika kusema kwamba sasa tumemaliza na kukamilisha mkataba wetu na Dowans na tupo tayari kuzalisha umeme hapa nchini…megawati 120 zinaweza kusaidia kupunguza matatizo ya umeme hasa ukizingatia kuwa nchi inakabiliwa na tatizo kubwa la mgawo wa umeme.”
Hata hivyo alisema wako tayari kuwasha mitambo hiyo ili ianze kazi mara moja, ila wanachongoja ni kuwasili kwa treni ya gesi ya Songosongo ilioharibika njiani.
akizungumzia kuhusu bei ya umeme watakayowauzia Shirika la Umeme nchini (TANESCO), alisema itakuwa nzuri na kwamba wanatarajia kuanza mazungumzo Jumatatu na kampuni hiyo kujadiliana namna ya kuanza kuwauzia umeme.
Naye Mwenyekiti wa Symbion Power Africa, Balozi mstaafu, Joseph Wilson aliongeza kuwa hata kama TANESCO hawata kuwa tayari kununua umeme kwao wanauwezo wa kuipeleka eneo lingine kwani kampuni hiyo inazalisha umeme maeneo mbalimbali ulimwenguni.